ARUSHA-Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Matride Kuyeto amewahakikishia abiria wanaosafiri kwa njia ya reli kuwa,Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wao wakati wote wa safari.
Akizunguma leo Desemba 2, 2025 katika Stesheni ya Reli ya jijini Arusha, ACP Kuyeto aliwahakikishia abiria wanaosafiri kutoka Arusha kuelekea Dar es Salaam kuwa njia ya reli ni salama na imeimarishwa kwa ulinzi wa kutosha.
“Niwahakikishie usalama katika safari yenu, na niwahakikishie kuwa mumechagua njia sahihi na salama ya usafiri wa reli kwa kuwa askari wetu wapo imara kabla na wakati wote wa safari mkiwa ndani ya treni,”amesema ACP Kuyeto.
Aidha, Kamanda huyo aliwahimiza abiria kuwa mabalozi wa amani katika jamii zao, akibainisha kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
Jeshi la Polisi Kikosi cha Reli limeendelea kuimarisha doria na ulinzi katika maeneo mbalimbali ya reli nchini, likilenga kutoa huduma salama na ya kuaminika kwa wasafiri.


