EWURA yatangaza bei mpya za mafuta mwezi Desemba,2025

DODOMA-Mamlaka ya Ushibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta aina ya petroli zitakazotumika hapa nchini kwa mwezi Desemba, 2025 huku zikionesha kuendelea kushuka kwa bei ya petroli.
Ahueni hiyo inatokana na kupungua kwa gharama za kuagiza mafuta katika bandari ya Dar es Salaam kwa wastani wa 2.4% kwa petroli, na 3.6% kwa mafuta ya taa.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Mwainyekule, tarehe 3 Desemba,2025, imebainisha kuwa, bei ya rejareja ya petroli imepungua kwa shilingi 2.38 (Dar es Salaam), 2.26 (Tanga) na shilingi 2.45 kwa Mtwara. Aidha, bei ya mafuta ya taa kwa Dar es Salaam imepungua kwa shilingi 120.48 ikilinganishwa na bei za mwezi Novemba 2025.

Hivyo basi, bei za reja reja za petroli kwa mwezi huu, zitakuwa shilingi 2610.10, 2616.13 na 2616.24 kwa Dar es Salaam, Tanga na Mtwara mtawalia. 

Kwa upande wa dizeli, Dar es Salaam ni shilingi 2639.54, Tanga 2648.86 na Mtwara 2654.32. Bei ya mafuta ya taa kwa Dar es Salaam ni shilingi 2513.87 huku bei za Tanga na Mtwara zikiwa hazina mabadiliko kutoka mwezi uliopita.

EWURA inawahimiza wauzaji wa mafuta nchini kutoa stakabadhi za mauzo kwa wanunuzi zinazoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita, kwani stakabadhi hizo hutumika kama kithibiti kunapokuwa na changamoto yoyote kuhusu huduma hiyo.

Aidha, EWURA inavikumbusha vituo vyote vya mafuta nchini kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei, punguzo na vivutio vya kibiashara. 

Pia,ni kosa kisheria kutoweka bango linaloonekana katika eneo la kituo na adhabu kali itatolewa kwa mujibu wa sheria kwa atakayekiuka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news