DODOMA-Katika siku za hivi karibuni, kumebainika utendaji usioridhisha katika Hospitali ya Temeke ikiwa ni pamoja na kuzimwa kwa mashine ya XRay, ambapo pia ufuatiliaji wa siri wa Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa umebaini uwepo wa rushwa za wazi wazi bila uoga.
Ni kuanzia kwa baadhi ya walinzi wasio waaminifu mpaka kwa baadhi ya watoa huduma na kauli mbaya zinazotolewa na walinzi hao na watoa huduma kwa wagonjwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 26,2025 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Wizara ya Afya, John Mapepele imefafanua kuwa,pia wamekuwa wakiwafokea wagonjwa na kuwadhalilisha kinyume na maadili ya kazi yao.
Kufuatia hali hiyo, Mhe. Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt.Seif Shekalaghe kufanya uchunguzi wa kina katika hospitali hiyo ili kubaini chanzo cha changamoto hizi na hatimaye kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni na sheria za utumishi kwa wale watakaobainika kuhusika ama kusababisha changamoto hizi.
Aidha, Mhe. Mchengerwa ametoa wito kwa watumishi wote wa Sekta ya Afya nchini kubadilika na kwamba Serikali haitasita kuchukua hatua kwa watumishi wazembe, wala rushwa au wanaokiuka misingi ya maadili ya kazi.
