HUDUMA YA MAJI:Kutoka kwenye huduma jamii hadi kichocheo kwa ukuaji wa uchumi

DODOMA-Maji si tu rasilimali ya msingi ya uhai wa viumbe hai na utunzaji wa mazingira, bali ni mtaji mkubwa unaochochea uchumi wa nchi na wananchi wenyewe katika maeneo mbalimbali ya kazi za kila siku.
Mama mjasiriamali wa maua akiongeza thamani ya soko kwa bidhaa zake kwa kutumia maji.

Tanzania, kupitia mabadiliko makubwa ya sera na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji, inafanya kazi ya kuwezesha maji kutoka kuwa huduma ya kijamii tu hadi kuwa chanzo cha kuinua kipato, kuimarisha kilimo, kukuza sekta mbalimbali na kulinda maisha ya mamilioni ya wananchi.

Mapema mwezi Machi 2025, Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002 (Toleo la 2025) na kuelekeza Wizara ya Maji kuendeleza utekelezaji wa Mpango wa Gridi ya Maji ya Taifa ili kuhakikisha usalama wa maji na usambazaji endelevu wa huduma hiyo nchini.

Hatua hiyo inaashiria uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu, uzalishaji, usambazaji na ulinzi wa vyanzo vya maji katika maeneo muhimu yanayochochea uchumi kupitia huduma ya maji.

Nchi ya Tanzania imepanga kuliweka suala la maji katika ajenda yake ya maendeleo. Kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 Serikali imeweka msingi thabiti wa kubadilisha mfumo wa huduma za maji kutoka katika mtazamo wa kuhudumia jamii pekee hadi kuwa nyenzo na chombo cha kiuchumi kinachoweza kuzalisha mapato, kuongeza ajira na kuvutia uwekezaji.

Sera ya Maji ni utekelezaji wa Dira lengo likiwa kuunganisha mipango ya kitaifa na ile ya kisekta/Wizara

Toleo jipya la Sera ya Maji linaweka kipaumbele katika usalama wa maji, ulinzi wa vyanzo vya maji, uwekezaji wa umma na binafsi (PPP), pamoja na uimarishaji wa taasisi za sekta.

Mwelekeo huu unakusudia kukuza utoaji huduma bora na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, jambo muhimu kwa nchi yenye malengo ya kujenga uchumi wa viwanda na kilimo usiotegemea masuala ya asili ya mvua pekee.

Mfano halisi wa uwekezaji unaolenga uchumi wa maji ni Mradi wa Mabadiliko ya Tabianchi Simiyu, unaotekelezwa kwa fedha za msaada wa Green Climate Fund (GCF), Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na Serikali ya Tanzania.

Mradi huu wenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 440 unalenga kuboresha usambazaji wa maji mijini na vijijini, kuongeza uzalishaji wa kilimo hata katika vipindi visivyo na mvua pamoja na kuimarisha miundombinu ya majisafi na usafi wa mazingira.

Utekelezaji wake umeongeza upatikanaji wa huduma za maji safi na salama kwa wananchi, huku ukichochea uchumi wa eneo husika kupitia kilimo, biashara na ajira.

Kupitia utekelezaji wa mradi huu, maelfu ya wananchi wamenufaika na ajira, biashara ndogo zimekua, na kipato cha wananchi kimeongezeka katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara.

Pamoja na hayo, hatua zilizochukuliwa na Serikali za ujenzi wa miradi mikubwa ya kitaifa ya maji kama mradi wa maji wa Mugango–Kiabakari–Butiama, upanuzi wa mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini, pamoja na miradi ya maji ya miji midogo na vijijini, ni kielelezo thabiti kwamba taifa linaelekea kwenye uchumi wa maji.

Kupitia mfano wa miradi kama hii na mingine mingi, faida za kiuchumi zinapatikana katika hatua tatu: za papo kwa papo ikiwamo ajira na biashara ndogo,za muda wa kati (tija ya kilimo na afya bora) na ajira za muda mrefu (huduma ya uhakika ya majisafi na salama, kuimarika kwa mazingira na usalama wa chakula).

Ni jambo lililowazi kuwa, huduma ya maji inageuka kuwa mtaji unaorejesha riba kwa jamii na taifa.

Tafiti na ripoti za kimataifa na kitaifa zinaonesha kuwa kuboresha huduma za maji ni njia thabiti ya kukuza uchumi.

Mashirika ya kimataifa ikiwa Shirika la Afya na Watoto, katika tafiti WHO/UNICEF Joint Monitoring Programme inabainisha kuwa dunia inaendelea kuongeza upatikanaji wa huduma za maji, ingawa bado changamoto ipo kwa mamilioni ya watu, hali inayopunguza tija ya uzalishaji na kuathiri afya ya jamii.

Marejeo ya Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka 2025/2026 inaonesha kuwa huduma za maji mijini zimefika zaidi ya wastani wa asilimia 91.6, huku vijijini zikifiia zaidi ya wastani wa asilimia 83 mwezi Disemba, 2024.

Takwimu hizi zinaashiria ufanisi mkubwa wa uwekezaji wa Serikali na wadau katika Sekta ya Maji ili kuifikia jamii.

Kila shilingi inayowekezwa katika huduma za maji inaleta faida kubwa za kiuchumi kupitia ongezeko la muda wa uzalishaji, kupungua kwa gharama za matibabu na kuondosha baadhi ya changamoto za afya, na uboreshaji wa kilimo na biashara ndogondogo.

Haya ni mafanikio makubwa yanayodhihirisha kwamba uwekezaji katika maji si tu wa kijamii, bali ni uwekezaji wa kiuchumi unaolipa kwa kiwango kikubwa kwa kuleta tija katika afya na ustawi wa jamii.

Aidha, Sekta ya Maji imeendelea kuwa chanzo kikuu cha ajira na mapato kwa maelfu ya Watanzania.

Kila mradi wa maji unaotekelezwa unahusisha makundi anuwai ya jamii wakiwamo wataalam washauri, wahandisi, mafundi, wauzaji wa vifaa na wakandarasi wadogo, wadau wa biashara ndogo ndogo, jambo linalothibitisha kuwa uwekezaji katika maji una mchango mkubwa wa moja kwa moja katika ukuaji wa ajira na biashara.

Kwa upande wa viwanda, upatikanaji wa maji ya uhakika ni kichocheo cha uwekezaji mpya, hasa katika sekta za vinywaji, chakula, ngozi, nguo na ujenzi.

Vivyo hivyo, maji yana mchango mkubwa katika Sekta ya Kilimo, ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.

Umwagiliaji wa uhakika unawawezesha wakulima kuzalisha kwa tija, kuongeza kipato, na kupunguza utegemezi wa mvua ambao umepitwa na nyakati.

Sera ya Maji ya Taifa yenye mwelekeo wa kibiashara inahimiza ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika huduma za maji, uzalishaji wa nishati kupitia maji, na huduma za teknolojia ya maji.

Hii imefungua fursa kwa kampuni za ndani na nje kuwekeza katika teknolojia za kutibu maji, mifumo ya kutoa taarifa kuhusu huduma ya maji (SCADA), mita janja (smart metering), na miradi ya udhibiti wa mtiririko wa maji ya mito pamoja na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Pamoja na ubunifu huo, zipo changamoto ikiwemo uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa vyanzo vya maji, na athari za mabadiliko ya tabianchi hususan suala la ukame na mafuriko yasiyotabirika.

Hivyo, utekelezaji wa programu za ulinzi wa vyanzo, uhifadhi wa ardhi na mazingira pamoja na teknolojia rafiki za maji, ni muhimu ili kujenga mfumo unaostahimili mabadiliko ya hali ya hewa.

Sekta ya Maji nchini Tanzania imepiga hatua kubwa ya kimapinduzi ikiwamo kuwa na Sera ya Maji, Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji.

Hatua hizi zimewezesha uwepo wa fursa za uzalishaji, ajira na huduma bora kwa wananchi na jamii kwa ujumla.

Kimsingi, utekelezaji wa hatua hizi umeweza kuonesha matokeo yenye mwanga kwa Sekta ya Maji kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi, kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi, huku ukihakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa vizazi vya sasa na vijavyo, na kujali mazingira.

Tanzania ipo katika njia sahihi ya kuibadilisha Sekta ya Maji kuwa injini ya uchumi endelevu kwa Serikali ya Awamu ya Sita kuipa kipaumbele Sekta ya Maji, sera nzuri, uwekezaji wa kifedha, teknolojia sahihi na ulinzi wa vyanzo vya maji, taifa lina nafasi ya kugeuza huduma ya maji kuwa injini ya maendeleo kwa sekta mbalimbali ikiwamo kilimo, viwanda, afya, utalii, nishati na mazingira.

Kwa uchache tunaweza kusema "Maji ni Uhai na Maji ni Uchumi”.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here