■ Wabainisha hayo walipomtembelea Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju
■Jaji Mkuu aipongeza Kamati hiyo kwa kazi nzuri
■Jaji Karayemaha, Mwenyekiti wa Kamati hiyo azitaka Kamati za Mikoa za Maadili ya Mawakili kutekeleza majukumu yao ipasavyo
NA MARY GWERA
Mahakama
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili, Mhe. James Karayemaha ametoa rai kwa Wadau kutoa ushirikiano kwa Kamati hiyo ili kufanikisha usikilizwaji wa jumla ya mashauri 45 ya mashauri ya kimaadili ya Mawakili wa Kujitegemea ambayo yamepangwa kushughulikiwa ndani ya siku 30.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyeketi mbele) akimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili, Mhe. James Karayemaha (wa kwanza mbele upande wa kushoto) wakati Kamati hiyo ilipomtembelea na kufanya mazungumzo na Jaji Mkuu ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma. Wengine ni sehemu ya Viongozi wa Mahakama (kulia) na Wajumbe wa Kamati hiyo.
Mhe. Karayemaha amebainisha hayo leo tarehe 17 Desemba, 2025 Ofisini kwa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma wakati yeye pamoja na sehemu ya Wajumbe wa Kamati hiyo walipomtembelea Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju kwa lengo la kujitambulisha na kueleza shughuli zinazofanywa na Kamati hiyo.
“Katika kutenda kazi zake, Kamati hii mpaka sasa inazo kesi 45 na mkakati wa kuzisikiliza kesi hizo umeshawekwa vizuri na utaanza tarehe 21 Januari, 2026 na tunatarajia mpaka mwezi wa 3 mwaka 2026 kesi zote 45 ambazo zimesajiliwa ziwe zimekwisha,” amesema Jaji Karayemaha.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mjumbe wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili, Mhe. Samwel Maneno (kushoto) akizungumza jambo wakati wa kikao cha majadiliano na Jaji Mkuu walipomtembelea ofisini kwake leo tarehe 17 Desemba, 2025. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili, Mhe. James Karayemaha.
Aidha, Mhe. Karayemaha ametoa wito kwa wote waliowasilisha kesi hizo kwenye Kamati wafike ili waweze kutoa ushahidi wao, wasikilizwe na hatimaye haki iweze kutendeka.
Ameongeza pia kwa kutoa wito kwa wale ambao wanalalamikiwa watakapopewa wito wafike kwenye Kamati ambayo Ofisi zake zipo kwenye Jengo la Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.
“Kwa wale ambao wameleta malalamiko au maombi na ambao hawatafika Kamati kwa kutumia vifungu vya kisheria itafuta malalamiko yao au maombi yao, kwahiyo tunaomba sana mfike. Na wale Mawakili ambao wamelalamikiwa kama hawatafika, Sheria inaruhusu Kamati kusikiliza kesi hiyo upande mmoja, kwa hiyo ni rai yangu kama Mwenyekiti wa Kamati hii, kuwaomba nyote mfike mtakapopewa wito na kesi yako imepangwa tarehe tafadhali fika ili kesi yako iweze kusikilizwa,” amesisitiza Mhe. Karayemaha.
Kadhalika, Mwenyekiti huyo ametoa rai kwa wananchi wanaokumbana na changamoto kutoka kwa Mawakili kuwasilisha malalamiko yao kwenye Kamati hiyo ili yaweze kushughulikiwa.
Amezitaka pia Kamati za Mikoa za Maadili ya Mawakili kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuwa Kamati hizo zimeanzishwa ili kuwapunguzia usumbufu wananchi. Amesema, takwimu walizo nazo zinaonesha kuwa, Kamati hizo hazifanyi kazi yoyote isipokuwa watu wanawasilisha malalamiko yao moja kwa moja kwenye Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili.
Akizungumzia kuhusu Rufaa kutoka kwenye Kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo amemueleza Jaji Mkuu kuwa, mpaka sasa kuna rufaa sita ambazo tatu zipo Mahakama Kuu na tatu nyingine zipo Mahakama ya Rufani ya Tanzania.
Wakiendelea na majadiliano.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akifuatilia kwa makini kinachojiri wakati wa mazungumzo kati yake na Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili iliyomtembelea leo tarehe 17 Desemba, 2025 ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Kuhusu mafanikio ya Kamati hiyo, Mwenyekiti amesema ni pamoja na kusikiliza mashauri kwa haki bila kupendelea upande mmoja na kutoa uamuzi haki, kusikiliza mashauri kwa wakati hasa yale ambayo wadaawa wamefika mbele ya Kamati, kusikiliza kesi bila kubanwa sana na kanuni za kisheria (legal technicalities) ili kuweza kutenda haki kwa wote wanaojua sheria na wasioijua sheria.
Ametaja mafanikio mengine kuwa, ni pamoja na kuendeleza mahusiano mazuri na wadau kama vile Mahakama na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kusuluhisha baadhi ya migogoro.
Mbali na mafanikio, Jaji Karayemaha amesema kwamba, Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili inakabiliwa pia na changamoto kadhaa ambazo ni pamoja na ukosefu wa bajeti, kukosa kanzidata na nyingine ambazo ameeleza kwamba jitihada mbalimbali zimefanywa na Kamati hiyo ili kutatua changamoto hizo.
Akizungumza mara baada ya kupokea Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili, Jaji Mkuu ameipongeza Kamati hiyo kwa kazi nzuri wanayofanya katika utekelezaji wa majukumu yao na kuwaahidi kuendeleza ushirikiano kati ya Mahakama na Kamati hiyo.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili waliomtembelea leo tarehe 17 Desemba, 2025 ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma. Wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili, Mhe. James Karayemaha, wa pili kushoto ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mjumbe wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili, Mhe. Samwel Maneno, wa kwanza kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert na wa kwanza kulia ni Katibu wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili ambaye pia ni Mwanasheria wa Serikali, Bw. Faraji Ngukah.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili waliomtembelea leo tarehe 17 Desemba, 2025 ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma. Wa tatu kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili, Mhe. James Karayemaha, wa tatu kushoto ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mjumbe wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili, Mhe. Samwel Maneno, wa pili kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili Mwandamizi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sundi Fimbo, wa pili kulia ni Katibu wa Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili ambaye pia ni Mwanasheria wa Serikali, Bw. Faraji Ngukah na wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili na Mkurugenzi wa Maktaba Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Kifungu Kariho.(Picha na MARY GWERA, Mahakama).
Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili ni chombo kilichoundwa kisheria ili kusimamia Maadili ya Mawakili wa Kujitegemea. Kamati hii imeanzishwa chini ya Sheria ya Mawakili Sura ya 341 Marejeo ya mwaka 2023.
Kwa mujibu wa Jaji Karayemaha, Kamati hiyo ina mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri yote ya kimaadili ya Mawakili wa Kujitegemea Tanzania bara.
Mashauri hayo ni pamoja na; Maombi ya Wakili mwenyewe kuomba jina lake kuondolewa katika orodha ya Mawakili, maombi ya mtu mwingine kuomba jina la Wakili fulani kuondolewa katika orodha ya Mawakili na kusikiliza mashauri ya kimaadili ya Mawakili wa Kujitegemea.






