Kampuni ya Bima ya Milembe yaamuriwa kumlipa fidia askari WP Asia Mtopa shilingi milioni 64.5 na riba ya asilimia saba

DAR-Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru Kampuni ya Bima ya Milembe kulipia fidia kwa askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani,Asia Salum Mtopa ya shilingi milioni 64,485,000 na ongezeko la riba ya asilimia saba ikiwa ni fidia ya kupata ajali iliyopelekea majeraha mbalimbali mwilini kwa askari huyo.
Hukumu hiyo imetolewa Disemba 22,2025 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,Rahim Mushi baada ya kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa na mleta maombi kwenye shauri hilo Asia Mtopa.

Ni shauri lililofunguliwa mahakamani hapo, akiwakilishwa na mawakili wasomi wawili Baraka Asajile na Stephen Kachemu kwenye kesi ya madai namba 1857/2024 dhidi ya wadaiwa Abbymeleky Jai Muhunzi na James Katsen Katumba pamoja na Kampuni ya Bima ya Milembe.

Awali katika kesi ya msingi ilyofunguliwa kwenye Mahakama hiyo waleta maombi hayo waliwasilisha ombi la kulipwa fidia ya shilingi 113,000,000 kama fidia ya gharama za matibabu na majeraha ya ujumla baada ya mteja wao akiwa amepakiwa kwenye pikipiki MC 482 aina ya HONLG akielekea kazini kugongwa na gari lenye namba za usajili T.194 CCD basi aina ya Isuzu iliyokuwa ikiendeshwa na Abbymeleky Muhunzi.

Hata hivyo, baada ya kusikikiza pande zote mbili Hakimu Mushi aliridhishwa na utetezi huo na kuamuru wadaiwa kulipa kiwango hicho cha fedha za Kitanzania kumfidia askari huyo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kutokana na majeraha aliyopata na gharama za matibabu.

"Nimesikiliza upande wa utetezi na walalamikiwa na baada ya kupitia hoja za pande zote mbili pasipo na shaka nimeridhika na hoja za waleta maombi na kuwaamuru kumlipa mleta maombi fidia ya Tsh. 64,485,000 pamoja na riba ya asilimia 7 ya fedha hiyo."

Katika shauri hilo upande wa walalamikiwa walikuwa wakitetewa na mawakili watatu Mngumi Samadandi, Jamaldin Ngolo na Manzie Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news