ZANZIBAR-Watendaji wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) wametakiwa kufanya kazi kwa ufanisi na umakini ili kuleta mafanikio chanya katika utekelezaji wa majukumu yao.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria na Utawala Bora, Dkt. Haroun Ali Suleiman, wakati akizungumza na wafanyakazi wa Ofisi ya DPP katika ofisi zao za Miembeni, akiwa katika ziara ya kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara yake.
Dkt. Haroun amesema kuwa ufanisi kazini ni miongoni mwa misingi mikuu ya kufanikisha malengo ya taasisi, hali itakayosaidia kuacha alama chanya na kuifanya Ofisi ya DPP kuheshimiwa na taasisi nyingine za Serikali.
Ameongeza kuwa ili kufikia ufanisi huo, wafanyakazi wanapaswa kujiendeleza kielimu ili kuongeza upeo wa kitaaluma na kufanya kazi kwa weledi, akisisitiza kuwa elimu ni nyenzo muhimu katika kufikia malengo ya taasisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Mheshimiwa Mgeni Jeilani Jecha, amesema Ofisi yake imetekeleza mikakati mbalimbali ya miaka 2022–2025, ikiwemo kuunda vikosi kazi vya kupambana na uhalifu mkubwa wa kupanga na makosa ya kifedha, hatua inayolenga kusaidia nchi kujiondoa katika orodha ya kijivu ya FATF.
Aidha, amesema Ofisi imeratibu kwa ufanisi upelelezi na uendeshaji wa kesi za madawa ya kulevya, rushwa na uhujumu uchumi, hali iliyopelekea kuongezeka kwa upatikanaji wa hatia katika kesi za madawa ya kulevya pamoja na kufanikiwa kutaifisha mali zitokanazo na uhalifu huo.
Mheshimiwa Jecha ameongeza kuwa Ofisi inakamilisha mfumo wa kidijitali wa uendeshaji wa mafaili ya kesi za jinai, utakaosaidia kupima utendaji wa wanasheria kulingana na idadi na ufanisi wa mafaili wanayoyawasilisha.
Vilevile, amesema Ofisi inakamilisha mfumo wa kupokea malalamiko ya wananchi, ambao utawezesha wananchi kuwasilisha malalamiko yao na kufuatilia mwenendo wa ushughulikiaji wake kuanzia hatua ya awali hadi kufikia mwisho wa kesi.
Ameeleza pia kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Ofisi ya DPP imejiwekea mikakati ya kufanya mageuzi katika utoaji wa mafunzo na miundombinu ya Kituo cha Sheria na Utafiti, ikiwemo kuboresha mitaala na kuwaendeleza walimu ili waweze kutoa elimu kwa ufanisi na weledi zaidi.
