MWANZA-Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limeendelea na zoezi la kutoa elimu kwa madereva na abiria, sambamba na kufanya ukaguzi wa magari, hususani mabasi ya masafa marefu yanayotoka nje ya Mkoa, ikiwa ni juhudi za kupunguza ajali na kuhakikisha usalama barabarani.
Zoezi hilo limefanyika leo Disemba 16,2025, katika Stendi ya Mabasi ya Nyegezi na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza, ACP Lwelwe Mpina, ambaye amesema lengo la ukaguzi huo ni kuhakikisha magari yako katika hali nzuri, madereva wanazingatia sheria za usalama barabarani, na kuwalinda abiria dhidi ya ajali zinazotokana na uzembe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, SSP Sunday Ibrahim, amesema ukaguzi huo ni wa mara kwa mara na ni sehemu ya operesheni endelevu ya kuhakikisha magari yote yanayofanya safari ndefu yanakaguliwa kabla ya kuondoka.
Amesema baadhi ya mabasi yalibainika na hitilafu ndogo ndogo zilizotatuliwa kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari.
Madereva wa mabasi ya masafa marefu wametakiwa kuwa na madereva wawili kwa kila safari ndefu, kudumisha nidhamu, lugha nzuri kwa abiria na kutii sheria za barabarani ili kulinda amani na usalama wa wasafiri.
Aidha, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu kwa umma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa usafirishaji, huku likisisitiza kuachana na tabia hatarishi kama mwendo kasi, kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhri na kukimbilia abiria, mambo ambayo huchangia kwa kiwango kikubwa ajali za barabarani.Mwenyekiti wa Rasilimali Watu katika Stendi ya Nyegezi, Daniel Damas, amesema matumizi ya tiketi za kielektroniki yameleta uwazi mkubwa na kudhibiti ongezeko holela la nauli.
Naye mmoja wa madereva, Omar Luqman, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa jitihada za kutoa elimu ya usalama barabarani na ameliomba Jeshi hilo kuedelee na kampeni hizo mara kwa mara ili kuongeza uelewa kwa wadau wote wa usafirishaji.



