ARUSHA-Wachimbaji wadogo wa madini ya Green Garnet katika eneo la Lemshuku Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini na taasisi zake kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia ili kubaini kiwango, ubora na thamani halisi ya madini hayo yanayopatikana katika maeneo wanayofanyia shughuli za uchimbaji.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 16, 2025 na Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wadogo Mkoa wa Manyara (MAREMA) eneo la Lemshuku Swalehe Abdalah wakati akizungumza na timu ya Madini Diary walipotembelea eneo la uchimbaji wa madini hayo.
Swalehe ameeleza kuwa, kwa muda mrefu wamekuwa wakichimba madini hayo kwa kutumia mbinu za jadi bila msaada wa tafiti za kitaalamu, hali inayowafanya kushindwa kutambua maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini na kukosa taarifa sahihi kuhusu thamani ya madini hayo katika soko la ndani na nje ya nchi.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo, Mkurugenzi wa kampuni ya Perfect, Godson Shoo amesema kuwa, kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi wamekuwa wakichimba bila kuwa na muongozo wa taarifa sahihi za kiutafiti kutoka kwa wataalam jambo ambalo linawapelekea kuchimba kwa kubahatisha kutokana na mazingira yalivyo ambapo inawapelekea kutumia muda mrefu na gharama nyingi.
Shoo ameongeza kuwa, endapo tutafanyiwa utafiti wa kitaalamu utasaidia kubaini aina na ubora wa madini ya Green Garnet (Tsavorite) hususan kwenye kujkwamahali, kina na ukubwa wa rasilimali iliyopo pamoja na kuboresha usalama kazini na uhifadhi wa mazingira.
Ameongeza kuwa, kukosekana kwa taarifa kuhusu na masoko na thamani ya madini hayo kumesababisha wachimbaji wengi kuuza madini yao kwa bei ndogo kupitia madalali, hali inayowanyima fursa ya kunufaika ipasavyo na rasilimali hiyo.
“Endapo utafanyika utafiti wa madini haya utatuwezesha kufanya uchimbaji wenye tija, kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo ya machimbo,” amesema Shoo.
Naye, Swalehe Said mfanyabiashara wa madini ya green garnet kwa miaka zaidi 10 ameiomba Serikali kushirikiana na Taasisi ya (GST) pamoja na wadau wa Sekta ya Madini kutoa mafunzo ya kitaalamu, kuwezesha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira ili kusaidia upatikanaji wa masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi ili wafanyabiashara wa kitanzania wanufaike na mnyororo mzima wa thaman madini.
Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya madini wanasema kuwa madini ya Green Garnet yana soko kubwa la vito duniani, hivyo utafiti wa kina na usimamizi mzuri vinaweza kuongeza mchango wa madini hayo katika uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wachimbaji wadogo.



.jpg)


