DAR-Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amewataka wananchi kuepuka matumizi holela ya dawa hususani antibiotiki kwani zinapotumika bila kufuata taratibu ujenga usugu na kushindwa kutibu ugonjwa.
Dkt. Magembe ametoa wito huo leo Disemba 2, 2025 wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Kanda ya Africa ya Wiki ya Kimataifa ya Usugu wa Vimelea vya Magonjwa Dhidi ya Dawa yanayoendelea jijini Dar es Salaam.Maadhimisho hayo ya Saba yanaendelea jijini Dar es Salaam na kuzikutanisha nchi mbalimbali kutoka Bara la Afrika kwa lengo la kubadilishana uzoefu kulingana na hatua iliyofikiwa na mataifa hayo.
Aidha, Dkt. Magembe amezitaka jamii kuzingatia usafi wa mazingira ikiwemo wakulima na wafugaji kutotiririsha maji yenye dawa kati vyanzo vya maji yanayotumika katika shughuli nyingine za kiuchumi na matumizi mengine ya binadamu.
Dkt. Magembe amewataka wakulima na wafugaji nchini kuacha matumizi holela ya dawa katika kilimo na ufugaji kwani matumizi yake ndiyo yanasababisha usugu wa dawa.

"Tuepuke kabisa matumizi holela ya dawa, dawa ni tiba,lakini ukiitumia vibaya bila utaratibu na maelekezo ya daktari unapata usugu na maana yake hiyo dawa haitakutibu tena,hivyo unalazimika kutumia dawa nyingine zenye gharama ya juu kukabiliana na ugonjwa husika,"aliongeza Dkt. Magembe.
Dkt.Magembe amezitaja juhudi za Serikali katika kukabiliana na matumizi holela ya dawa kuwa ni kuwepo kwa kamati ya ufuatiliaji matumizi holela ya dawa lakini pia kampeni maarufu "Holela Holela itakukosti".
Dkt. Magembe amezitaja juhudi nyini kuwa ni kuwepo kwa Dawati lijulikanalo kama Afya moja lenye lengo la kufuatilia matumizi anwai ya dawa linalosimaiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kama mratibu ili kuhakikisha wadau wote wa Afya serikalini wanawajibika kuzingatia matumizi bora ya dawa akiitaja sekta ya kilimo na maeneo mengine.





