Mgongolwa afunguka mazito, awataja vijana,CNN na CCM

IRINGA-Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Iringa,Joseph Mgongolwa amewataka vijana nchini kutambua kuwa wana dhamana kubwa katika kuhakikisha amani na utulivu vinadumu, huku akiwataka kuimarisha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwao.

Lengo ni kulinda ustawi wao,Taifa na kulinda maadili ya kijamii ambayo ni msingi wa maendeleo endelevu.
Mgongolwa ametoa rai hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Iringa baada ya kuona baadhi ya watu na makundi yenye nia ovu wanajitahidi kuvuruga amani ya taifa kwa manufaa yao binafsi, kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025.

"Hali hii inaathiri sio tu usalama wa nchi, bali pia inachangia kuzorotesha maendeleo, na kuleta mgawanyiko miongoni mwa wananchi.

"Vijana wana jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba tunadumisha amani na umoja wetu, kwa kuwa sisi ni viongozi wa kesho,"amesema Mgongolwa.

Amesema, vijana wanapaswa kuwapuuza watu wenye nia ovu ya kuvuruga utulivu wa nchi, kwani wao wanatumia mifumo ya kijamii na kisiasa kama njia ya kujinufaisha kiuchumi au kisiasa.

Mgongolwa ameongeza kuwa, vijana wana nafasi ya kipekee katika kujenga taifa lenye mshikamano na wanapaswa kuwa na dhamira ya kujenga si kuharibu.

Pia, amewahimiza vijana kutojihusisha na makundi ya kihalifu au yale yanayochochea vurugu kwa maslahi yao binafsi.

"Mtu yeyote anayekusudia kutenganisha umoja wetu ni adui wa Taifa na ni jukumu letu kuhakikisha hatutoi nafasi kwa watu hawa,amani ya Taifa letu ina thamani kubwa sana kwetu sisi Watanzania na Dunia itatutazama sisi kama Taifa lenye heshima kubwa."

Katika hatua nyingine, Mgongolwa anasema vyombo vya habari vya kimataifa vinaitendea ndivyo sivyo Tanzania, hususan CNN kupitia ripoti yake ya karibuni baada ya kuandika taarifa ambazo amedai kuwa na upendeleo kuhusu uchaguzi mkuu wa Tanzania uliofanyika Oktoba 2025.

Ripoti hiyo ya CNN, inayotokana na picha za satellite na vyanzo vya habari vya nje, imeelezwa kuwa ilijikita zaidi katika kuonesha mapungufu, huku ikipuuzilia mbali mafanikio yaliyopatikana katika mchakato wa uchaguzi.

"Si jambo la heri na haliungwi mkono na Mtanzania yoyote. Ripoti ya CNN kuhusu uchaguzi wa Tanzania imeegemea upande mmoja, na haijatoa nafasi kwa serikali kusema chochote kuhusu hatua zilizochukuliwa ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.

"Taarifa za namna hii hazina manufaa kwa taifa letu, bali zinachochea migawanyiko na uvunjifu wa amani,"amefafanua Mgongolwa.

Aidha,kuna wasiwasi kwamba vyombo vya habari vya kimataifa mara nyingi huzingatia upande mmoja wa tukio, na kutengeneza picha ya hali ya nchi kulingana na mtazamo wao, badala ya kutoa picha kamili na yenye mizania.

Hii inakuwa na athari kubwa kwa jamii za kimataifa, hasa wakati wa migogoro au mizozo ya kisiasa, ambapo matokeo ya taarifa zisizokuwa na usawa yanaweza kuleta athari kubwa kwa amani ya kitaifa.

Mgongolwa amesisitiza kwamba,vyombo vya habari vya kimataifa vinatakiwa kuwa na uwazi na haki katika kuripoti matukio ya kijamii na kisiasa, na kuepuka kuandika habari zinazoweza kuchochea machafuko na kuvuruga amani ya taifa.

"Tunahitaji kuona taifa letu likistawi, si kusambaratika,"amesema Mgongolwa wakati akizungumzia jinsi vyombo vya habari vinavyoweza kuathiri hali ya kisiasa na kijamii kupitia uandishi wa habari usio wa haki.

Vilevile, Mgongolwa amesitiza umuhimu wa vyombo vyote vya habari kuzingatia miongozo ya kitaifa ya uandishi wa habari, ili kulinda maslahi ya taifa na kuhakikisha kwamba taarifa zinawasilishwa kwa umakini na usawa.

Pamoja na changamoto zinazojitokeza, Mgongolwa amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kusimama imara na kuisemea serikali, hasa kwa kuzungumzia mafanikio ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Wanachama wa CCM tusiwe mabubu, tunapaswa kuungana kwa lengo moja la kulinda na kuendeleza mafanikio ya kitaifa.

"Tunasimama kidete katika kuleta maendeleo kwa wananchi, na lazima tuonyeshe mafanikio ya Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan," amesema Mgongolwa wakati akizungumzia umuhimu wa kuzungumzia miradi mikubwa iliyotekelezwa na inayotekelezwa katika sekta mbalimbali kama vile miundombinu, afya, elimu, maji na michezo.

Amesema, Rais Dkt.Samia na serikali yake wameendelea kutekeleza miradi mikubwa kama vile ujenzi wa barabara za kiwango cha kimataifa, miradi ya umeme vijijini, huduma za maji,uwekezaji katika sekta ya afya na mingineyo, ambayo imekuwa na athari chanya kwa maendeleo ya wananchi.

Mgongolwa anasisitiza kuwa ni muhimu kwa chama hicho kuungana na kuonesha umoja ili kuhakikisha kwamba miradi hii inatekelezwa kwa mafanikio.

Hata hivyo,vijana nchini wanapaswa kutambua jukumu lao la kihistoria katika kulinda na kudumisha amani na umoja wa kitaifa.

Ikumbukwe hii ni dhamira ambayo inapaswa kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku, huku wakiepuka kushiriki katika mivutano ya kisiasa inayoweza kuleta madhara kwa jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news