Rais Dkt.Samia aendelea kuwapigania wakulima:Msaada wa Dola Milioni 9.38 kuikomboa Mkondoa dhidi ya mafuriko na ukame

MOROGORO-Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika diplomasia ya maendeleo na usimamizi wa uchumi kwa vitendo.
Hivi karibuni, Mfuko wa Maendeleo wa Afrika (African Development Fund) umeidhinisha ufadhili wa takribani dola za Marekani milioni 9.38 kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa Tanzania kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika Bonde la Mto Mkondoa.

Ufadhili huu umetolewa kupitia dirisha maalum la Climate Action Window, hatua inayohakisi imani na heshima kubwa ambayo taasisi za kimataifa zinaendelea kuiweka Tanzania kutokana na sera madhubuti, diplomasia shirikishi na uongozi thabiti wa Rais Dkt.Samia.

Mradi huu unalenga kulinda maisha ya wananchi, kuimarisha shughuli za kilimo na kuhifadhi miundombinu muhimu dhidi ya athari za mafuriko na ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Mradi huu una lengo la kulinda jamii zilizo hatarini na miundombinu muhimu kutokana na mafuriko na ukame unaosababishwa na hali ya hewa inayobadilika.

Aidha,manufaa makuu ya mradi ni kulinda maisha na biashara za wakulima dhidi ya mafuriko na ukame.

Pia,kuimarisha mifumo ya tahadhari mapema na ujenzi wa miundombinu imara dhidi ya hali ya mabadiliko ya tabianchi kama vizingiti na mabwawa madogo.

Faida nyingine ni urekebishaji na kurejesha ardhi hekta 1,200 zilizoharibika ikiwemo kufungua fursa za ajira takriban 3,500 kazi za muda na 1,000 ajira za kudumu, hasa kwa wanawake na vijana. ⁠

Vilevile,mradi utaleta faida kwa wanaume, wanawake na familia 774,000 wanaoishi katika wilaya za Gairo, Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro.

Mradi huu utatekelezwa na Wami/Ruvu Basin Water Board chini ya Wizara ya Maji, na kazi itaanza Januari,2026.

U⁠natarajiwa kuboresha usalama wa maji kwa matumizi ya kaya na kilimo, kupunguza umaskini, kuimarisha usalama wa chakula na kusaidia ukuaji wa uchumi endelevu pamoja na kulinda barabara ya kimkakati ya Morogoro–Dodoma (B-127).

Kupatikana kwa ufadhili huu ni ushahidi wa mafanikio ya diplomasia ya kiuchumi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ambapo Tanzania imefanikiwa kujenga ushirikiano imara na wadau wa maendeleo, kuvutia rasilimali za kimataifa, na kuelekeza misaada hiyo kwenye miradi yenye tija kwa maendeleo ya wananchi.

Pia, mradi wa mto Mkondoa unaonesha kwa vitendo dhamira ya Rais Dkt.Samia ya kuhakikisha maendeleo endelevu, ulinzi wa mazingira, na ustawi wa wananchi vinaenda sambamba.

Hiki ni kielelezo tosha kwamba uongozi makini, diplomasia yenye tija na sera bora za kiuchumi vinaweza kuleta matokeo chanya yanayogusa maisha ya watu moja kwa moja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here