ANKARA-Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari alifanya mazungumzo na ujumbe kutoka Jumuiya ya wenye Viwanda na Wafanyabiashara nchini Uturuki (MÜSIAD) jijini Ankara, Desemba 16, 2025.
Ujumbe huo uliokuwa na jumla ya viongozi na watendaji sita uliongozwa na Mjumbe wa Bodi na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uhusiano wa Kidiplomasia MÜSIAD, Bw. Osman Nuri Önügören ulitembelea Ubalozi kwa lengo la kuimarisha ushirikiano mzuri na kuibua fursa zaidi kwenye sekta za biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili.
Kwa upande wake, Balozi Iddi aliishukuru Jumuiya hiyo kwa ushirikiano mzuri kwa Tanzania na aliwakaribisha wawekezaji kutoka Uturuki kuwekeza nchini kwenye zao la pamba ambalo linazalishwa kwa wingi na nchi ya Uturuki imeendelea zaidi kwenye teknolojia na viwanda katika sekta hiyo.
Mazungumzo hayo yalifikia azma ya Ubalozi kukutana na Bodi ya Wadau wa Pamba mapema Januari,2026 ili kufanya majadiliano ya kina yatakayowezesha kuwaunganisha wadau wa pamba wa pande zote mbili kuanza mazungumzo ya ushirikiano kwa maslahi ya pande zote mbili.
Ni dhahiri kwamba fursa hiyo itafungua soko, uwekezaji, teknolojia na uongezaji thamani wa zao la pamba kwa kuwaunganisha wadau husika kutoka Uturuki na Tanzania.
Aidha, Ubalozi utaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa makubaliano hayo ili kuhakikisha nchi inanufaika vyema kupitia diplomasia ya uchumi yenye tija kwa manufaa ya wananchi wake.


