NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa ufafanuzi kwa kina huku akifichua siri nzito kuhusu matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025 huku.

Katika mkutano na Baraza la Wazee wa Jiji la Dar es Salaam leo Desemba 2,2025 jijini humo,Rais Dkt.Samia amesema, kilichotokea hakikuwa maandamano halali bali ni vurugu na machafuko yaliyopangwa kwa dhamira ya kuipindua Serikali.
“Twende na ukweli. Haya hayakuwa maandamano. Kuunguza miradi ya Serikali, vituo vya polisi, vituo vya mafuta, magari na biashara za watu si maandamano. Hizi zilikuwa vurugu zilizoandaliwa kwa madhumuni maalum ya kuiangusha Serikali,"amesema Rais Dkt.Samia.

Ameongeza kuwa, Serikali ililazimika kutumia nguvu kulingana na ukubwa wa tukio, akisisitiza kuwa hakuna taifa duniani linalokubali mipango ya kuvuruga amani likabaki kimya.
“Tuliapa kulinda mipaka, raia na mali zao. Mnataka tukae tu mpaka wapate walichotumwa? Dola haiendeshwi hivyo."
Rais Dkt.Samia amesema,Dar es Salaam haiwezi kuruhusiwa kuwa kitovu cha vurugu kwa kuwa ndicho kinachoakisi taswira ya Tanzania duniani, huku asilimia 10 ya Watanzania wakiishi katika mkoa huo.
“Tutasimama imara. Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo,"amesema huku akisisitiza kuwa,mchakato wa Katiba Mpya haujapingwa na Serikali, akibainisha kuwa tayari mambo mengi ya muda mfupi na wa kati yaliyopendekezwa na Tume ya Haki Jinai yameanza kutekelezwa.
Pia,Rais Dkt.Samia ameeleza kuwa,sehemu kubwa ya vijana walioshiriki vurugu hizo hawakufanya hivyo kwa sababu ya ugumu wa maisha bali kwa sababu walilipwa au walifuata mkumbo.
“Kama ni ugumu wa maisha, ningeweza ningewapeleka nchi nyingine waone ugumu ukoje. Wenye shida ya kweli hujishughulisha kutafuta riziki, si kuingia barabarani kuimba woyooo...,”amesema.
Sehemu ya Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 02 Desemba, 2025.Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema,Serikali imeunda Wizara mpya ya Vijana ili kushughulikia changamoto na kuongeza uzalendo kwa kundi hilo muhimu.
Vilevile,Rais Dkt.Samia ametoa wito kwa taasisi za dini kutovuruga amani kwa matamko yanayoweza kuathiri mshikamano wa kitaifa.
“Tanzania haina dini,Watanzania wana dini. Hakuna dhehebu lililopewa mamlaka ya kutoa tamko kwa niaba ya wote. Tangu nimekaa madarakani, TEC wametoa matamko manane, na hata wao kwa wao wanapingana,"amesema.Katika hatua nyingine,Rais Dkt.Samia amekanusha madai kuwa, Serikali imezuia vyama vya upinzani kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 29,2025.
“Hatujawazuia. Kama kuna madai, meza ya mazungumzo ipo.Hakuna sababu ya kuchochea vurugu,”amesema.
Sehemu ya Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 02 Desemba, 2025.
Sehemu ya Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 02 Desemba, 2025.Ameongeza kuwa, baadhi ya waratibu wa vurugu wanaishi nje ya nchi na wanawatumia Watanzania waliokosa uzalendo kutimiza dhamira na malengo yao.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Salum Matimbwa amempongeza Rais Dkt.Samia kwa uamuzi wa kuunda Tume ya uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29 na kuagiza kuachiwa kwa vijana waliojiingiza katika vurugu bila kuelewa madhara.
“Tumeona vijana wengi wameachiwa na kurejea majumbani. Tunamshukuru Rais kwa hekima hii,”amesema.
Aidha, wazee wamempongeza Rais kwa kuunda Wizara ya Vijana na kwa ahadi ya bima ya afya kwa wazee ndani ya siku 100 za awamu yake ya uongozi.
Sehemu ya Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 02 Desemba, 2025.Matimbwa amesema, wazee wana imani kuwa Tanzania itaendelea kuwa kisiwa cha amani chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia, licha ya changamoto zilizojitokeza wakati wa uchaguzi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri,manaibu waziri,maafisa waandamizi pamoja na wazee kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
