DAR-Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesitisha kibali cha udahili na usajili wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Udaktari wa Binadamu kwa Chuo Kikuu Mwanza (MzU) kwa mwaka wa masomo 2025/2026.

Ni kwa kubainika kukiuka taratibu za udahili ambapo Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema, uamuzi wa TCU umefikiwa mara baada ya kufanya ukaguzi wa awali ambao ulibaini chuo hicho kimedahili na kusajili idadi ya wanafunzi mara 10 zaidi ya ile iliyoidhinishwa na mamlaka hiyo.
TCU imeeleza kuwa kabla ya kufikia uamuzi huo ilitoa maelekezo kwa Chuo Kikuu cha Mwanza kufanya marekebisho ya idadi ya wanafunzi waliodahiliwa, lakini chuo hicho kilishindwa kufanya marekebisho ambayo kwa mujibu wa tume ya idadi ya wanafunzi waliosajiliwa ni kubwa kuliko rasilimali zilizopo chuoni hapo.


