Rais Dkt.Samia aongoza waombolezaji kuaga mwili wa Jenista Joakim Mhagama

DODOMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo ameongoza familia, viongozi, wabunge na waombolezaji katika ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mhe. Jenista Joakim Mhagama, iliyofanyika katika Kanisa la Mwenyeheri Maria-Theresa Ledochowska, Parokia ya Kiwanja cha NdegeJimbo Kuu Katoliki Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiongoza waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Marehemu Jenista Joakim Mhagama, katika ibada iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu la Dodoma, tarehe 13 Desemba 2025.

Rais Dkt. Samia ameeleza masikitiko makubwa ya Taifa kufuatia msiba huo, akimwelezea marehemu kuwa alikuwa kiongozi jasiri, mwaminifu na mlezi wa viongozi wengi ndani ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyelitumikia Taifa kwa moyo wa kujitoa, nidhamu, uadilifu na hofu ya Mungu, akisimama imara kutetea haki,
maendeleo na usawa wa wananchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na waombolezaji mara baada ya ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Marehemu Jenista Joakim Mhagama, katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu la Dodoma, tarehe 13 Desemba, 2025.
Aidha, alitambua mchango mkubwa wa Marehemu akihudumu kwa ufanisi katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali na Chama cha Mapinduzi, sambamba na uwezo wake wa kubeba majukumu mazito kwa weledi.

Akigusia urithi wa uongozi aliouacha, Rais Dkt. Samia alisisitiza kuwa moyo wake wa kujali maslahi ya Taifa ndio nguzo kuu ya kumbukumbu ya Hayati Jenista Mhagama, na
kutoa wito kwa wabunge na viongozi wote kuiga mfano wake wa maadili na uwajibikaji
aliouonesha.

Halikadhalika, Rais Dkt. Samia aliwataka viongozi kuuenzi mchango wa Marehemu kwa
kuimarisha misingi ya uwajibikaji, mshikamano wa kitaifa na utumishi unaolenga maslahi mapana ya wananchi.
Rais Dkt. Samia alitoa pole kwa familia, ndugu, wananchi wa Jimbo Peramiho, Bunge na Taifa kwa ujumla, na kumuomba Mwenyezi Mungu awape faraja, nguvu na amani, huku akiiombea roho ya Marehemu pumziko la amani ya milele.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news