Serikali itaongeza bajeti ya elimu hadi shilingi trilioni 1-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali ina mpango wa kuongeza bajeti ya sekta ya elimu kutoka shilingi bilioni 864 hadi kufikia shilingi trilioni 1, ili kuimarisha ubora wa elimu nchini.
Akizungumza leo Disemba 5, 2025 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 13 wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari za Zanzibar (JUWASEZA) uliofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Fidel Castro, sambamba na ufunguzi wa Dakhalia mpya ya wanafunzi wa kike iliyopo Mkoa wa Kusini Pemba, Dkt. Mwinyi alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuboresha mazingira ya ufundishaji, maslahi ya walimu pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kielimu.
Amesema,ujenzi wa Dakhalia hiyo ni sehemu ya mkakati maalum wa Serikali wa kuimarisha sekta ya elimu, akibainisha kuwa mpango ni kujenga Dakhalia katika kila wilaya ili kufikia idadi ya wanafunzi 10,000 watakaosoma katika skuli za Dakhalia ifikapo mwaka 2030.

Aidha, Rais Mwinyi amewataka walimu wakuu kusimamia ipasavyo miundombinu ya elimu, ufaulu wa wanafunzi na rasilimali za umma, huku akiahidi kutenga fedha maalum kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu pale inapohitajika. 

Pia,amewahakikishia walimu kuwa Serikali itaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwinyi ameahidi kuyapitia upya maslahi ya walimu wastaafu na watumishi wengine wa umma, ikiwemo suala la nyumba bora, pensheni na posho, kwa lengo la kuboresha ustawi wao.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Lela Mohamed Mussa, amesema mageuzi yanayoonekana katika sekta ya elimu yanatokana na maono na juhudi kubwa za Rais Mwinyi katika kusukuma maendeleo ya elimu Zanzibar.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdallah Said, akiwasilisha taarifa ya kitaalamu, amesema ujenzi wa Dakhalia ya wasichana ya Skuli ya Fidel Castro umegharimu shilingi bilioni 1.5 na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 288, kwa wastani wa wanafunzi 28 kwa kila darasa. Ameongeza kuwa wizara inatarajia kujenga Dakhalia nyingine 16 Unguja na Pemba katika mwaka wa fedha 2025–2026.

Mradi huu wa Dakhalia ya wanafunzi wa kike wa Skuli ya Fidel Castro ndio wa kwanza kufunguliwa na Rais Dkt. Mwinyi kisiwani Pemba tangu kuchaguliwa tena kuiongoza Zanzibar kwa kipindi cha pili cha Awamu ya Nane.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news