Serikali ya Awamu ya Nane kipindi cha pili inahitaji kasi ya utekelezaji,uwajibikaji na usimamizi bora wa majukumu-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane Kipindi cha Pili inahitaji kasi ya utekelezaji, uwajibikaji, na usimamizi bora wa majukumu ili kupata matokeo chanya katika kuwahudumia wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Disemba 11, 2025 alipofungua Mafunzo ya Awali kwa Viongozi Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, yaliyofanyika katika Chuo cha IIT Madras, Bweleo huko Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kwamba mafunzo hayo yana lengo la kuimarisha usimamizi bora wa utendaji, kuongeza uwajibikaji, na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alieleza kuwa viongozi hao wanapaswa kuvipa kipaumbele vipengele sita muhimu ili kufanikisha malengo ya Serikali na kuleta mabadiliko chanya.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa ni muhimu kwa Watendaji Wakuu wa Serikali kuwa na uelewa wa juu wa mbinu za kisasa za kuongeza ufanisi na kasi ya utendaji, huku akisisitiza matumizi bora ya takwimu katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa ufanisi.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kutumia mifumo ya kidijitali na kuongeza ufanisi katika taasisi za umma, kuimarisha usimamizi wa watumishi, na kuendeleza nidhamu ya utumishi wa umma.
Alieleza kuwa, wakati umefika kwa viongozi wa Serikali kuimarisha mikataba ya utekelezaji na usimamizi wa majukumu ili kupata matokeo bora.

Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza viongozi hao kuwa na ratiba ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, kuhakikisha hakuna mradi unakwama, na kufanya ufuatiliaji wa ahadi za Serikali kwa wananchi, hasa zile zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kupata uzoefu na stadi mpya zitakazowawezesha kuongeza uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kuimarisha uongozi bora katika taasisi za Serikali.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), na ni ya kwanza kufanyika kwa Watendaji Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news