Serikali yatangaza vipaumbele vipya vya Uwekezaji na fursa kwa vijana katika utekelezaji wa Dira 2050


OFISI ya Rais, Mipango na Uwekezaji (OR-MU) imetangaza mpango mpana wa mageuzi ya kiuchumi, kisera na kiutendaji unaolenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji.
Sambamba na kuongeza fursa za ajira kwa vijana nchini katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kuelekea utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji,Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb) ameyabainisha hayo leo Desemba 8,2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Katika mkutano huo,Prof.Mkumbo ameeleza kwa kina mwelekeo wa Serikali katika kuimarisha sekta ya uwekezaji, kuboresha utendaji wa mashirika ya umma, na kukamilisha maandalizi ya nyenzo kuu za utekelezaji wa Dira 2050.

Prof.Mkumbo amesema kuwa,katika kipindi cha 2021 hadi 2025, jitihada za Serikali zimechangia ongezeko kubwa la miradi ya uwekezaji na mtaji nchini.

Amesema,miradi iliyosajiliwa imeongezeka kutoka miradi 252 mwaka 2021 hadi miradi 901 mwaka 2025 na mtaji ulioingia nchini umeongezeka kutoka dola za kimarekani bilioni 3.7 mwaka 2021 hadi dola bilioni 9.3 mwaka 2024.

Prof.Mkumbo amesema kuwa,uratibu wa shughuli hizo unaongozwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), ambayo itaendelea kuwa kiungo muhimu katika kuvutia wawekezaji na kuimarisha mazingira ya biashara nchini.

Kuhusu,hatua kuu za kuimarisha uwekezaji nchini mwaka 2025 hadi 2030, Prof.Mkumbo amesema,Serikali imepanga kuchukua hatua muhimu ikiwemo kuimarisha Kituo cha Mahala Pamoja (One Stop Centre).

Amesema,kituo kina taasisi 14 zinazotoa huduma muhimu kwa wawekezaji mahala pamoja ili kuondoa urasimu ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), NEMC, OSHA, Uhamiaji, TBS, TANESCO, TMDA, NIDA na Wizara ya Ardhi.

Jambo la pili ni kuanzisha na kuendeleza Benki ya Ardhi ambapo hadi sasa TISEZA inamiliki zaidi ya hekta 170,000 kwa ajili ya uwekezaji, zikiwemo SEZ 34, mashamba na maeneo maalum ya kiuchumi.

"Kwa mujibu wa Sheria Na. 6 ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi ya Mwaka 2025, TISEZA imepewa jukumu la kuanzisha benki ya ardhi kwa kushirikiana na wizara yenye dhamana ya ardhi pamoja na mamlaka za serikali za mitaa.

"Hadi sasa, TISEZA inamiliki ardhi yenye ukubwa wa Hekta 170,176.96 kwa ajili ya uwekezaji, ikijumuisha mashamba na maeneo maalum ya kiuchumi."

Pia, amesema hatua nyingine ni kuanzisha Jukwaa la Taifa la Uwekezaji (National Investment Forum) ambapo kuanzia Januari 2026, litaratibiwa na TISEZA likihusisha mawaziri na wawekezaji ili kufanya tathmini, kupokea changamoto na kuboresha mazingira ya uwekezaji.

"TISEZA itakuwa na jukumu la kuratibu jukwaa hili ambalo litahusisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Fedha, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri wa Muungano na Mazingira na taasisi husika za umma ili kukutana na wawekezaji kwa dhumuni la kufanya tathmini ya maendeleo ya uwekezaji nchini, kusikiliza changamoto, kupokea maoni, na kuyafanyia kazi."

Amesema,miradi itapewa kipaumbele kwa kuzingatia uwezo wa kuzalisha ajira, kuongeza mauzo nje, kuongeza thamani, kuchochea sekta nyingine na kukuza mapato ya serikali.

Kuhusu kipaumbele cha Sekta 10 za Uwekezaji, Prof.Mkumbo amesema,Serikali itahimiza uwekezaji katika kilimo na uchakataji,uzalishaji wa bidhaa tunazoagiza nje (madawa, mafuta ya kula, ngano),ufugaji na uvuvi na uchakataji wa samaki.

Nyingine ni utalii,ujenzi,madini,huduma za fedha,misitu,nishati, ikiwemo mafuta na gesi.

Vilevile, amesema Serikali imeweka mkazo maalum kwa vijana kama injini ya uchumi wa Dira 2050.

Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na Kuanzisha Kituo Maalum kwa Wawekezaji Vijana (Youth Investors Resource Centre) na Programu ya Taifa ya Viwanda kwa Vijana.

Waziri Mkumbo amesema,vijana waliomaliza vyuo watapewa maeneo maalum kuanzisha viwanda katika maeneo ya Dodoma (Nala- ekari 100),Pwani (Kwala-ekari 20),Mara (Bunda-ekari 100),Ruvuma (Songea-ekari 100) na Bagamoyo-ekari 20).

Amesema,programu itatoa mafunzo, ardhi, unganishi kwa mitambo na malighafi, na kuwaunganisha na benki kama Azania, TCB, na CRDB.

Aidha, amesema jambo lingine ni kupanua huduma za uwekezaji hadi ngazi ya mikoa kufikia mwaka 2028 na ujenzi wa Industrial Shades kwa Ubia na Sekta Binafsi.

Prof.Mkumbo amesema,miundombinu hii itapangishwa kwa gharama nafuu ili kupunguza gharama za kuanzisha viwanda.

Pia,kubuni vivutio vipya vya uwekezaji ili kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la dunia.

Mbali na hayo, Prof.Mkumbo amesema,Tume ya Taifa ya Mipango inaandaa nyenzo kuu tatu za kuanza utekelezaji wa Dira 2050 kuanzia Julai, 2026

Mosi ni Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP I-Dira 2050),pili ni Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Mwaka Mmoja, ADP 2026/2027 na tatu ni Mfumo wa Ufuatiliaji na Upimaji Matokeo (RBMELA Framework)
Mageuzi ya Mashirika ya Umma.

Amesema,Serikali inakamilisha muswada wa Sheria mpya ya Uwekezaji wa Umma, ambayo itajumuisha mfumo mpya wa kupima utendaji wa mashirika kwa kuzingatia tija na utoaji huduma.

Masharti ya mashirika ya kibiashara kujisajili katika Soko la Hisa (DSE) na utaratibu wa kupata viongozi kwa ushindani na uwazi.

Aidha, amesema, jambo lingine ni kuanzishwa kwa chanzo maalum cha fedha cha kutekeleza miradi ya uwekezaji wa umma.

Waziri Prof.Mkumbo amesema, Serikali inataraia ifikapo 2030 ajira milioni 8 kuzalishwa kupitia miradi ya uwekezaji na mtaji wa angalau dola bilioni 50 kuvutiwa nchini

Sambamba na kuimarika kwa ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kupitia KPIs na mashirika ya umma kuongeza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma na mchango katika uchumi.

"Ni matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwa ifikapo mwaka 2030, hatua kubwa zitakuwa zimepigwa na mafanikio makubwa kupatikana, ikiwemo miradi ya uwekezaji kuongezeka, fursa za ajira kupanuka na mitaji ya uwekezaji kukua.

"Matarajio ni kuzalisha ajira milioni nane na kuvutia mtaji wenye jumla ya dola za Kimarekani angalau bilioni 50 ifikapo 2030.

"Kuimarika kwa usimamizi, ufuatiliaji na upimaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vigezo vya matokeo (Key Performance Indicators-KPIs).

"Kila wizara na taasisi ya umma itapewa viashiria vya kufikia na watapimwa kwa kuzingatia viashiria hivyo,"amefafanua Waziri Prof.Mkumbo.

Kuhusu OR-MU

Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji (OR MU) ilianzishwa Julai 2023 ikiwa na jukumu la kuratibu uandaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa na kuandaa na kusimamia utekelezaji wa sera zinazohusina na uwekezaji nchini.

Aidha, ofisi hii ina jukumu la kuratibu na kusimamia utendaji wa taasisi tatu za umma ikiwemo Tume ya Taifa ya Mipango (National Planning Commission-NPC), Ofisi ya Msajili wa Hazina (Treasury Registra-TR), na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (Tanzania Investment and Special Economic Zones Authority – TISEZA).

Tume ya Taifa ya Mipango (NPC) ina jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kitaifa, ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.

Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) ina jukumu la kutunga na kusimamia utekelezaji wa miongozo kwa mashirika ya umma. Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) ina jukumu la kuratibu, kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news