DAR-Kampuni ya Ulinzi ya SGA Security kwa mara nyingine imetajwa kuwa mtoa huduma za usalama anayeaminika zaidi barani Afrika, na kutwaa tuzo ya chaguo la mtumiaji kwa mwaka 2025 (Consumer Choice Awards Africa 2025).
Tuzo hiyo ilitangazwa kwenye Tamasha la Tuzo ya Chaguo la Mtumiaji Afrika kwa mwaka 2025 kwenye Ukumbi wa SuperDome, Masaki, Jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, na mamia ya makampuni kutoka Bara la Afrika.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Tanzania, Dk Eric Sambu, alisema kwamba mara nyingine watumiaji wa huduma za kampuni yao wameonesha imani kwa kampuni kongwe ya ulinzi katika bara la Afrika.
Tuzo hiyo ya SGA inakuja baada ya tuzo nyingine ya awali kwa Kampuni Bora ya Ulinzi ya Mwaka Afrika katika Kundi la Huduma za Ulinzi.
Akieleza zaidi, alisema SGA imewekeza katika kuwaridhisha wateja wake, hivyo imekuwa ikiboresha huduma zake ili kuhakikisha wateja wake wanapata thamani ya fedha katika mahusiano yenye manufaa kwa pande zote mbili.
Aliongeza kwamba tuzo hiyo ni kwa ajili ya wafanyakazi wote, ambao ni zaidi ya 18,000 katika bara la Afrika, ambao kila mwaka huwahudumia wateja wao vizuri, na kuongeza juhudi katika utoaji wa huduma.
"Tuna vyeti vinne vya Shirika la Kimataifa la Kusanifisha (ISO), ambavyo vimepatikana kwa miaka kadhaa, vikionyesha matengenezo ya mifumo thabiti ya usimamizi ili kuhakikisha ubora wa huduma zetu kwa manufaa ya wateja wetu na kwa umma," aliongeza.
Kwa mujibu wa Dk Sambu, siri ya mafanikio katika huduma za ulinzi ni kuwawezesha wafanyakazi kuwahudumia wateja vizuri, na kwamba kampuni yao imewekeza sana katika kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa ngazi zote, hasa juu ya mienendo, na vitendo vinavyojitokeza, na hatari ya vitisho.
Tuzo ya Chaguo la Mtumiaji Afrika ni tukio la kila mwaka linalolenga kutoa tuzo kwa makampuni, mashirika na taasisi barani Afrika katika sekta mbalimbali za uchumi kupitia maoni ya umma yanayokusanywa kama kura za mtandaoni kupitia tovuti hii, iliyoanzishwa mwaka 2019 Jijini Dar es Salaam, Tanzania.
