Serikali itaendelea kutatua changamoto za watu wenye ulemavu nchini-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukua hatua za kimkakati kuhakikisha changamoto zinazowakabili Watu Wenye Ulemavu nchini zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Akizungumza leo Desemba 3,2025 katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein uliopo Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, Rais Dkt. Mwinyi ametangaza kuwa, Serikali itaendelea kuhakikisha Watu Wenye Ulemavu wanapata haki za kijamii, kisiasa, na kiuchumi bila ubaguzi. Alihaidi kuwa hakuna mlemavu atakayekosa fursa ya kujiendeleza katika jamii.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ametaja hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali, akisema kuwa Serikali inazingatia mahitaji maalum ya Watu Wenye Ulemavu katika ujenzi wa miundombinu kama vile hospitali, skuli, ofisi za umma, na barabara.

Kwa mfano, alisema kuwa Serikali imejenga skuli mbili maalum kwa wanafunzi wenye ulemavu katika Mkoa wa Kusini Unguja na Pemba, na kwamba inakusudia kujenga skuli nyingine tatu katika mikoa mingine.

Pia, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutoa ruzuku, vifaa saidizi, mafunzo, na mikopo isiyo na riba kwa watu wenye ulemavu ili kuwasaidia kiuchumi na kujitegemea.

Amewahimiza wananchi na jamii kwa ujumla kuwasajili watoto wote wenye ulemavu ili waweze kupata vifaa bure kutoka kwa Serikali.

Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kutoa mikopo isiyo na riba kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) pamoja na fedha za uwiano kutoka Serikali za Mitaa kwa Watu Wenye Ulemavu ili kuwasaidia kuimarisha maisha yao.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi amewashukuru wadau wa ndani na wa kimataifa kwa ushirikiano wao katika kusaidia Watu Wenye Ulemavu, na alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau hao ili kupata suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazowakabili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here