Sheria ya Uwekezaji wa Umma mbioni, Prof.Mkumbo aipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imesema kuwa, ipo mbioni kuja na sheria mpya ya Uwekezaji wa Umma ili kuhakikisha mashirika ya umma yanaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na yanachangia kikamilifu katika Pato la Taifa.
Hayo yamebainishwa Desemba 5,2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Mheshimiwa Prof.Kitila Mkumbo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara yake katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) jijini Dar es Salaam.

"Na kazi yangu kama Waziri ni kuhakikisha kwamba, tunasimamia maelekezo ya Mheshimiwa Rais katika mageuzi hayo ambayo anayataka,na kwa sasa, kazi yangu kubwa ni kuwapatia hawa sheria nzuri ya kusimamia Uwekezaji wa Umma.

"Tupo katika hatua za mwisho, tunatarajia kwamba sheria mpya ya Uwekezaji wa Umma iweze kufikishwa katika Baraza la Mawaziri muda mfupi ujao na hatimaye iende bungeni."

Amesema,tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ni wajibu wake kuzitembelea taasisi zilizopo chini ya ofisi yake ili kuzipa mwelekeo kama alivyofanya katika Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Kwanza ninataka niwapongeze Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kazi kubwa ambayo mmefanya na mafanikio makubwa ambayo tumeyapata mwaka huu ni katika maeneo mawili."

Mosi, Prof.Mkumbo amesema,ni kuongeza mchango wa mashirika ya umma katika mapato ya Serikali ambapo kwa mwaka huu waliweza kufikisha zaidi ya shilingi trilioni moja.

Amesema, lengo ambalo wamepewa mwaka 2025-26 ni kufikisha angalau shilingi trilioni 1.7.

"Ndiyo lengo ambalo Serikali imewapa na ni jukumu langu kusimamia kuhakikisha kwamba kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, mashirika yanatekeleza hilo."

Jambo la pili, Prof.Mkumbo amesema, Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikisimamia mageuzi ambayo Serikali imeagiza yafanyike katika mashirika yote ya umma.

Amesema,mageuzi hayo yapo katika maeneo makubwa mawili ikizingatiwa yapo mashirika ya umma 308 kati ya hayo, kuna mashirika ya umma ambayo hayafanyi biashara na yanayofanya biashara.

Waziri Mkumbo amesema kuwa, lengo la Serikali ni kuona mashirika ya umma yanaendelea kuwa sura ya Serikali katika utoaji huduma, lakini pia kuwa sura ya Serikali katika Uwekezaji wa Umma na wanataka kuhakikisha mashirika ya umma yanaendelea kufanya vizuri katika maeneo hayo.

Ili yafanye vizuri, Waziri Mkumbo amesema, wanafanya mageuzi makubwa ikiwemo upande wa utendaji wao ili mashirika ya umma yaweze kuboresha na kuimarisha utendaji.

"Ni ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi, kwa sababu Serikali inatoa huduma kupitia mashirika ya umma kama ni afya ni kupitia hospitali zetu. Kama ni elimu ni kupitia shule na vyuo vyetu,kwa hiyo ni eneo ambalo tunataka tuliboreshe.

"Lakini, la pili mashirika ya umma ni sura ya Serikali, na sura ya umma katika Uwekezaji wa Umma, Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi trilioni 90 na tunataka uwekezaji huu uweze kuzaa kwa maana ya kuendelea kujenga uwezo wa Serikali katika kutoa huduma za kiuchumi."

Amesema, kupitia eneo hilo ndiyo maana wanafanya mageuzi makubwa katika utendaji na muundo wa mashirika ya umma kama wanavyokuja na Sheria ya Uwekezaji wa Umma.

Vilevile amesema,Serikali itaongeza ufanisi zaidi kwa kuhakikisha upatikanaji wa watendaji na wajumbe wa bodi za mashirika ya umma kupitia ushindani na uwazi.

Pia, amesema mashirika ya umma ambayo hayaoneshi ufanisi ikiwemo kutoa huduma bora kwa wananchi na kuwasilisha gawio sahihi kwa Serikali, hawatasita kuyafuta au kuyaunganishi ili kuongeza ufanisi zaidi.

"Jambo la muhimu ni kuona kuwa, yanabaki mashirika ya umma ambayo yana tija.Kama Shirika la umma linafanya biashara, tunataka kuona linafanya biashara na linatengeneza faida na linatoa gawio sahihi kwa Serikali."

Katika ziara hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina inayoongozwa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu imemshukuru na kumpongeza Waziri Prof.Mkumbo kwa ziara hiyo.

Mbali na pongezi hizo, pia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeyapokea maelekezo yaliyotolewa na Waziri ili kuimarisha utendaji wa ofisi hiyo.

Wizara hiyo inasimamia taasisi kubwa tatu za umma ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Hazina, Tume ya Taifa ya Mipango na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news