TAMKO RASMI LA UMOJA WA MAKANISA YA KITUME NA KINABII TANZANIA LA KUFUNGA MWAKA 2025 LEO DESEMBA 16,2025 MOROGORO,TANZANIA

NDUGU waandishi wa habari, awali ya yote,sisi viongozi wa Umoja wa Makanisa ya Kitume na Kinabii Tanzania tunamshukuru Mungu kwa baraka zake na kutupa nchi njema ya Tanzania.

Pia,tunamshukuru Mungu kwamba tangu tupate Uhuru miaka zaidi ya 64 iliyopita na baadaye Muungano wetu, taifa letu limeendelea kudumisha umoja, mshikamano wa kitaifa na amani, hali ambayo imeifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Vilevile, tunawashukuru ninyi waandishi wa habari na vyombo vyenu vya habari kwa kazi nzuri na kubwa ambayo mmekuwa mkiifanya katika kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha umma.

Ndugu waandishi wa habari, kanisa na Watanzania kwa ujumla tunayo furaha kuwaeleza kuwa, sisi Umoja wa Makanisa ya Kitume na Kinabii Tanzania tumeendelea kukua na kupanua huduma zetu kote mijini na vijijini.

Leo Desemba 16,2025 ninapozungumza nanyi hapa,tunamshukuru Mungu kuwa,umoja huu umepanuka na sasa tuna muungano wa madhehebu ya Kikristo zaidi ya 200 nchini.

Kupitia madhehebu hayo, kote nchini tuna matawi zaidi ya 15,000 ambayo yanaongoza mamilioni ya waumini kutoka ndani na nje ya nchi, huu ni ushindi mkubwa katika kuujenga mwili wa Kristo, hakika sifa na utukufu tunamrudishia Mungu.

Katika kuhakikisha taasisi hii ya Umoja wa Makanisa ya Kitume na Kinabii Tanzania inakuwa imara kuanzia kiimani na maadili mema, Mungu ametupatia wazee wengi kuwa walezi wa chombo hiki, kwa heshima kubwa naomba niwataje hawa watatu kwa niaba ya wengine.

Mosi ni Mtume Mkuu Dkt.Dastan Maboya, pili ni Nabii Mkuu Dkt.Geordavie na tatu ni Mzee wa Upako,Mchungaji Anthony Lusekelo kwa hekima na uzalendo wao kwa kiasi cha kuwa tayari kuifia nchi yetu kwa injili ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu awape maisha marefu na yenye heri sana hapa duniani.

Ndugu waandishi wa habari, naomba kwa kifupi sana niwaeleze namna huduma za Makanisa yetu zinavyofanya kazi.

Makanisa yetu ya Kitume na Kinabii yana huduma ndani yake ambazo ni Karama za Mungu na kila mmoja amepewa Ufunuo tofauti na wengine kama apendavyo Mungu mwenyewe aliye muokoaji wa wote.

Aidha, huduma hizi zimelenga kutatua matatizo ya watu bila ubaguzi wa kidini au itikadi yoyote ile, hivyo zimekua kimbilio la watu wa dini zote, wanasiasa na hata wasio na dini pia wamekuwa wakinufaika na huduma zetu hiI kwa namna moja au nyingine.

Ndugu watanzania wenzetu kutokana na aina hiyo ya wito wetu na utumishi wa Mungu kwa watu wote, tumeona tunawajibu mkubwa wa kuutimiza hasa kipindi hiki ambacho umoja na mshikamano wetu wa kitaifa umejaribiwa kiasi cha kusababisha maumivu makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa ndani ya mipaka ya nchi yetu njema ya Tanzania.

Ndiyo maaana leo Desemba 16,2025 tumekusanyika hapa mkoani Morogoro kama viongozi waandamizi wa umoja wetu na madhehebu mbalimbali ya kidini kutoka kila mkoa ili tuseme yafuatayo kwa ajili ya kuliponya na kulifariji taifa letu kwa yote yaliyotokea.

Kwanza, tunatoa pole tena na tena kwa wote waliofiwa na kuumia wakati wa vurugu zilizo tokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025 na tunalaani mambo kama hayo yasije yakatokea tena juu ya uso wa nchi yetu njema.

Pia, tunaipongeza Serikali kwa jitihada ilizozichukua kuhakikisha inatimiza wajibu wake wa kulinda raia na mali zao, japo kwa yaliyotokea tunaamini lipo la kujifunza kwa siku za usoni.

Aidha, kwa moyo wa unyenyekevu sana tunawaomba sana na kuwasihi vijana wa taifa letu kutambua kuwa,hii nchi ni urithi wao kutoka kwa Mungu,kwani walio kuwa msitari wa mbele na wa hatari zaidi wakati wa kupigania Uhuru walikuwa vijana wakiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na baadaye kule Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume.

Historia inatufundisha kuwa,mafanikio hayo ya vijana yalitokana na ushirikiano usiotiliwa shaka kati yao na wazee (baraka za wazee katika kufikia lengo ni njia nyoofu isiyo poteza mtu),naomba msituchoke niwape kisa kimoja katika Biblia.

Ukisoma Biblia Takatifu utaona Mfalme Ahabu alilitamani shamba la Nabothi,alimuomba Naboth amuuzie, lakini Nabothi alikataa kwa kuwa lilikuwa ndio shamba pekee la urithi wake.

Mfalme alifadhaika sana kwa kulikosa lile shamba, kisha akamweleza Yezebel mkewe, Yezebel akasema yeye atalichukua shamba hilo kwa njia ya kumkosanisha Nabothi na ndugu zake, akasema atatafuta watu wasiofaa wawe mashahidi wa uongo kuwa Nabothi amemtukana Mungu na mfalme,kisha nitawajulisha wakuu wa mji ili wamhukumu kifo,kisha watalichukua shamba hilo liwe miliki yao.

Ndugu zangu kisa hiki kinatoa fundisho kubwa sana kwa nchi yetu leo,ndugu zetu vijana wa Tanzania jueni kuwa, kwa sababu ya umoja wa kitaifa na mshikamano wetu wageni (mfalme mkoloni) walitamani nchi yetu na rasilimali zetu kwa muda mrefu bila mafanikio.

Hivyo,wakaona heri wawakodi wanaharakati wasiofaa (mayezebel) ili walifitinishe taifa na Serikali yao ambayo kikatiba ndiyo yenye dhamana ya kulinda rasilimali zetu,ili yakitokea machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe wao wapate urahisi wa kuingia kama wapatanishi ili wapore urithi wetu, kamwe tusikubali hila hizo mbaya katika taifa letu.

Ndugu watanzania wenzetu,bahati yetu nzuri mwezi huu ni wa 12, ni mwezi ambao kwa sisi Wakiristo tulio wengi tunasherehekea kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kiristo, ambaye kwa mujibu wa imani yetu yeye ndiye mfalme wa amani na mshauri wa ajabu.

Katika mandiko matakatifu, Bwana Yesu amewahi kusema mambo haya kati ya mengi kama ifuatavyo;

1:Amani iwe nanyi.

2:Iweni na umoja.

3:Samehe saba mara sabini.

4:Ushindeni ubaya kwa wema.

5:Amri kuu nawapa, nayo ni upendo.

6:Akunyang'anye kanzu mpe na shati.

7:Alirudishia sikio la askari lililokatwa akiwa anamkamata amsulubishe.

Ndugu zangu Watanzania,wakati huu wa Sikukuu ya Krismasi lazima tuzingatie tabia na uhalisia wa huyu tunayesherehekea kuzaliwa kwake,tukifanya hivyo mioyo yetu itapokea roho yake na kusambaza upendo miongoni mwetu, bila kuinajisi siku hii muhimu ya mfalme wa amani tukaitia doa la damu au machafuko.

Ndugu zangu vijana na watanzania, sisi viongozi wenu wa kiroho tunawasihi tena kwa mioyo iliyopondeka sana kuwa badala ya kuandaa maandamano basi tuandae siku ya sikukuu, iwe ni siku ya kumuomba Mungu na kutafakari njia bora ya kutatua changamoto zetu kama nchi bila ya kumwaga damu.

Sisi mitume na manabii nchini Tanzania, tunaamini ile roho ya Mungu iliyompa akili kijana Julius Kambarage Nyerere aliyepata Uhuru bila kumwaga damu,hatimaye tukampa heshima ya kuwa Baba wa Taifa, basi na sisi vijana wa leo tunaweza kuitumia sikukuu hii ya Desemba 25,2025 kukataa kabisa maandamano na kuamua kama mababa na wamama wa taifa la watoto wetu kesho.

Ndugu zangu,baada ya kusema hayo tunawashukuru kwa kupokea ujumbe wetu, Mungu ibariki Tanzania,Mungu wabariki vijana wa Tanzania hadi wasema basi kuandamana.

Kwa niaba ya Umoja wa Makanisa ya Kitume na Kinabii Tanzania,mimi ni mtumishi wa Mungu.

Dr Nabiijoshua Aram Mwantyala,
Rais wa Umoja wa Makanisa ya Kitume na Kinabii Tanzania.
Leo Desemba 16,2025.
Morogoro,Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news