NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewashauri wananchi na wadau wote kuendelea kufuatilia taarifa za mara kwa mara za hali ya hewa ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya mvua, hasa kwa shughuli za kilimo, uvuvi, usafiri na matumizi ya barabara nchini.
Wavuvi wanategemea sana taarifa za hali ya hewa ili kutekeleza majukumu yao ya kila siku majini.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 4,2025 na TMA ikiangazia mwenendo wa mvua kwa siku 10 zilizopita pamoja na matarajio ya hali ya hewa kwa siku kumi zijazo.
Kwa mujibu wa TMA, mwenendo wa viashiria na mifumo ya mvua kwa Novemba 21 hadi 30,2025 migandamizo mikubwa ya hewa iliyopo kaskazini mwa dunia (Azore na Siberia) iliendelea kuimarika wakati ile iliyopo kusini mwa dunia (St. Helena na Mascarene) iliendelea kudhoofika.
Pia, hali hii ilisababisha sehemu ya ukandamvua (ITCZ) kusogea kuelekea kusini na kuwepo katika maeneo ya ukanda wa ziwa Victoria, magharibi mwa nchi, nyanda za juu kusini magharibi na maeneo jirani, hali ambayo iliimarisha mifumo isababishayo mvua katika maeneo hayo.
Vilevile, uwepo wa upepo wenye unyevunyevu
uvumao kutoka baharini kuelekea maeneo ya ukanda wa pwani na maeneo jirani uliimarisha mifumo isababishayo mvua katika maeneo hayo hasa katika kipindi cha siku tano za mwanzo.
TMA, imebainisha kuwa, kulingana na viashiria tajwa vilipelekea uwepo wa vipindi vya mvua zilizoambatana na ngurumo za radi katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, magharibi mwa nchi, nyanda za juu kusini magharibi pamoja na maeneo ya kusini mwa nchi.
Pia, vipindi vya mvua katika maeneo machache ya ukanda wa pwani na nyanda za juu kaskazini mashariki.
Kuhusu matarajio ya hali ya hewa ikiwemo viashiria na mifumo ya mvua kwa Desemba 1 hadi 10,2025 TMA imebainisha kuwa,katika kipindi hiki, migandamizo mikubwa ya hewa iliyopo kaskazini mwa dunia (Azore na Siberia) inatarajiwa kuendelea kuimarika.
Aidha, ile iliyopo kusini mwa dunia (St. Helena
na Mascarene) inatarajiwa kuendelea kudhoofika.
TMA imefafanua kuwa,hali hii inatarajiwa kusababisha sehemu ya ukandamvua (ITCZ) kusogea kuelekea kusini na kuwepo katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, magharibi mwa nchi, nyanda za juu kusini magharibi na maeneo jirani, hali ambayo inatarajiwa kuimarisha mifumo isababishayo mvua katika maeneo hayo.
Vilevile, uwepo wa upepo wenye unyevunyevu uvumao kutoka baharini kuelekea maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi yetu unatarajiwa kuimarisha mifumo isababishayo mvua katika maeneo hayo hasa katika kipindi cha siku tano za mwisho.
Mbali na hayo, kuhusu mwelekeo wa mvua kwa Desemba 1 hadi 10,2025 TMA imefafanua kuwa, Kanda ya ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara) vipindi vya mvua zinazoambatana na ngurumo za radi vinatarajiwa katika maeneo machache hususan katika kipindi cha siku tano za mwisho.
Nyanda za juu kaskazini-mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), TMA imebainisha kuwa,hali ya ukavu kwa ujumla inatarajiwa.
TMA pia imefafanua kuwa,Pwani ya kaskazini (Mikoa ya Tanga, Maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) kunatarajiwa kuwa na vipindi vya mvua nyepesi katika maeneo machache hususan katika kipindi cha siku tano za mwisho.
Magharibi mwa nchi (Mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora) huku mvua zinazoambatana na ngurumo za radi zinatarajiwa katika maeneo machache ya mikoa ya Kigoma na Katavi hususan katika kipindi cha siku tano za mwisho.
Upande wa Kanda ya kati (Mikoa ya Dodoma na Singida), TMA imesema,hali ya ukavu kwa ujumla inatarajiwa huku Nyanda za juu Kusini-magharibi (Mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa) vipindi vya mvua vikitarajiwa katika maeneo machache hususan katika kipindi cha siku tano za mwisho.
Pwani ya kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi) nako vipindi vya mvua nyepesi vinatarajiwa katika maeneo machache hususan katika kipindi cha siku tano za mwisho.
Kanda ya kusini (Mkoa wa Ruvuma na Maeneo ya kusini mwa Morogoro), pia vipindi vya mvua vinatarajiwa katika maeneo machache hususan katika kipindi cha siku tano za mwisho.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania
