TRA yatoa msamaha wa adhabu kwa wamiliki wa vyombo vya moto vilivyokiuka sheria na taratibu za kiforodha

DAR-Mamlaka  ya Mapato Tanzania (TRA) imesema mwisho wa msamaha wa adhabu kwa wamiliki wa vyombo vya moto vilivyokiuka sheria na taratibu za kiforodha ni leo.

Vyombo hivyo ni magari, pikipiki na mitambo ambavyo vilibainika havikufanyiwa taratibu za forodha ambazo ni ushuru na kodi zake za uingizaji, hazikulipwa ipasavyo.

Msamaha huo ulitolewa na Kamishna wa TRA, kuanzia Agosti Mosi, 2025 na mwisho wake ukiwa leo.

Aidha, vyombo vinavyohusika katika msamaha huo ni vyombo vya moto vilivyoingizwa nchini kwa muda,lakini havikurudishwa nje ya nchi, vyombo vya moto kutoka Zanzibar vilivyoingia Tanzania Bara bila kuzingatia taratibu za forodha na vyombo vya moto vilivyopaswa kusafirishwa nje ya nchi,lakini vikatelekezwa.

Vingine ni vilivyopata msamaha na kuhamishwa kwa watu binafsi wasio na sifa ya kupata msamaha huo na vyombo vya moto vya kusafirishwa ambavyo muda wake wa kuwa nchini ulioidhinishwa uliisha bila kuongezewa kibali.

Katika kipindi cha msamaha huo, wamiliki waliostahili walitakiwa kulipa ushuru na kodi zilizobaki, huku riba, faini na adhabu zote zikifutwa kikamilifu.

TRA imesema chombo chochote kitakachokamatwa katika makundi yaliyotajwa au mengineyo ambayo ushuru na kodi zake hazikulipwa ipasavyo, baada ya Desemba 31, 2025 mmiliki wake atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Imesema mbali na hatua za jinai, ushuru na kodi, riba, faini na adhabu zitawekwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news