Tushirikiane kutokomeza ukatili mtandaoni-Mama Mariam Mwinyi

ZANZIBAR-Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Hussein Mwinyi ambaye pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), amesisitiza kuwa ukatili wa kijinsia, hususan unaotekelezwa mitandaoni, ni changamoto ya kijamii inayohitaji nguvu ya pamoja.
Amesema kuwa, katika dunia ya sasa teknolojia imeleta fursa nyingi, lakini pia imekuwa chanzo cha aina mpya za ukatili kama lugha za matusi, vitisho, kusambazwa kwa picha au taarifa binafsi bila ridhaa na uonevu wa kimtandao.

Mama Mariam Mwinyi amesema,aina hizi za ukatili zimekuwa zikiharibu maisha ya wanawake na wasichana na kupunguza ushiriki wao katika nafasi mbalimbali za maendeleo na uongozi.
Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo leo Disemba 6,2025 aliposhiriki katika Kongamano la Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia lililoandaliwa na Chama cha Majaji Wanawake (TAWJA) – Zanzibar, katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Aidha, amesisitiza kwamba mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia mtandaoni yanahitaji elimu endelevu kwa vijana, wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kuhusu usalama wa kimtandao.

Ametoa wito kwa Serikali, vyombo vya sheria, wataalamu wa teknolojia, vyombo vya habari na asasi za kiraia kuimarisha mifumo ya kisheria, kuongeza ufanisi katika kuripoti matukio ya ukatili, na kutoa huduma za msaada kwa waathirika ikiwemo msaada wa kisaikolojia na kijamii.
Akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya ZMBF, Mama Mariam Mwinyi ameonesha dhamira ya kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kunakuwepo na mazingira salama kwa kila mwananchi.

Kufikia sasa ZMBF imewafikia wanufaika 3,667 kwa kuwapa elimu, ushauri nasaha na huduma za kitabibu ikiwemo afya ya akili kwa waathirika.

Pia,kwa sasa inashirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutengeneza mfumo wa kidijitali utakaoweza kutoa taarifa, kutunza na kuratibu mwenendo wa kesi za udhalilishaji.

Vile vile ameipongeza TAWJA – Zanzibar kwa juhudi wanazoendeleza katika kukuza haki na usawa wa kijinsia, na kusema kuwa kongamano hilo ni fursa muhimu ya kuongeza ari na kasi ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Katika kuhitimisha, Mama Mariam Mwinyi amesisitiza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu “Tuungane Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia Mitandaoni” inataka hatua za pamoja na uwajibikaji wa kila mmoja, huku akihimiza umuhimu wa kutumia lugha njema mtandaoni, kulinda faragha ya wengine na kukataa kuwa sehemu ya mnyororo wa usambazaji wa taarifa za udhalilishaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news