Tutamuenzi kwa vitendo marehemu Jenista Joakim Mhagama-Waziri Mkuu

RUVUMA-Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itayaendeleza mambo yote mema yaliyofanywa na aliyekuwa mbunge wa Peramiho mkoani Ruvuma, Marehemu Jenista Mhagama ikiwemo kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kidini.
Amesema, marehemu Jenista alikuwa mpatanishi akiunganisha makundi mbalimbali yakiwemo ya wafanyakazi na Serikali ambapo hadi leo wanaushirikiano mkubwa, pia aliimarisha umoja na mshikamano kati ya Serikali na sekta binafsi na alifanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa.
“Marehemu Jenista amekuwa anaamini katika mafanikio na hiyo ndio iliyompa jina la kiraka kwa kuwa kila nafasi aliyopewa aliimudu kwa ukamilifu. Jenista amegusa maisha ya wengi, mimi nilikuwa nashirikiana naye katika masuala ya uongozi na alikuwa mmoja wa marafiki wa familia.”
Ameitoa kauli hiyo Desemba 15, 2025, wakati akiwasilisha salamu za Serikali aliposhiriki Ibada ya kuaga mwili wa Marehemu Jenista Mhagama iliyofanyika katika kanisa Katoliki la Abasia ya Mtakatifu Benedicto, Peramiho.

Katika salamu hizo, Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemuagiza awahakikishie Watanzania wakiwemo Wana-Ruvuma kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kama ilivyokuwa inafanya wakati wa uhai wa Jenista.
"Mheshimiwa Jenista alikuwa kiungo kati ya Wana-Ruvuma na Wana-Peramiho na alikuwa kiungo kati ya Kanisa na Serikali, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amenituma niwahakikishie wote kwamba Serikali itaendelea kuyaenzi mema yote aliyoyafanya enzi za uhai wake.”

Vile vile, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikisha watoto wa marehemu kwamba hawatakuwa peke yao, wataendelea kushirikiana nao, ambapo amewasisitiza watoto hao waendelee kumtanguliza Mwenyezi Mungu mbele huku wakishikamana na kupendana somo ambalo marehemu amewaachia.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Mussa Zungu amewashukuru viongozi wa Serikali na viongozi wa dini kwa kazi kubwa waliyoifanya tangu kutokea kwa msiba.

Awali, Victor Mhagama ambaye ni mtoto wa Marehemu Jenista ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa familia tangu kutokea kwa msiba huo huku akiiomba Serikali na wananchi kwa ujumla waendelee kuwa pamoja nao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news