MTWARA-Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mheshimiwa Abdallah Mwaipaya ameitaka jamiii kutofumbia macho na kukaa kimya pale wanapoona watu wanafanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Pia, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuelimisha na kukemea wananchi dhidi ya mila potofu ambazo zimekuwa zikichangia ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Mheshimiwa Mwaipaya amebainisha hayo Disemba Mosi,2025 katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini katika Kata ya Nanguruwe kwenye siku ya uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Amesisitiza kuwa,maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia yapaze sauti ili kukomesha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ambao bado ni changamoto kubwa katika jamii zetu.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia Wilaya ya Mtwara,Mkaguzi msaidizi Juliana Chenge amesema, maendeleo ya sayansi na teknolojia hususani matumizi ya mitandao ya kijamii yameleta matokeo chanya kama vile ajira.
Pia yameleta matokeo hasi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa zenye kutweza utu, hivyo kufanya wahalifu kutumia mitandao hivyo kutengeneza fursa za kiuchumi kwa kuwanyanyasa watu kisaikolojia.
Amesitiza kuwa, endapo mtu atanyanyasika kupitia mitandao ya kijamii asisite kutoa taarifa kupitia kitengo maalumu cha makosa ya kimtandao ndani ya Jeshi la Polisi.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwa ni pamoja na mtandao wa Polisi wanawake Mtwara kufanya matendo ya huruma kwa kumsaidia gharama za matibabu ya shilingi 500,000 kwa mtoto anayepitia changamoto ya ulemavu.












