DAR-Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW) leo Desemba 18,2025 kimewajengea uelewa wanafunzi na wahitimu wake katika kuhakikisha wanatumia Akili Unde (AI) ipasavyo ili kuwa msaidizi muhimu katika kuweza kuchaka na kurahisisha kazi zao.
Akizungumza wakati wa Kongamano la 17 lililozungumzia Matumizi ya Akili Unde kwenye uwanda wa taaluma ya Ustawi wa Jamii,Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dkt.Joyce Nyoni ametoa wito wa kuacha kuongopa kutumia AI kujifunza.
Dkt.Nyoni amewataka kuitumia AI kama msaidizi ambaye ataweza kuwasaidia kuchakata kazi zao, lakini sio kwamba itachukua nafasi ya kazi zao.
"Tumekutana kuona ni kwa namna gani tunaweza kuitumia akili unde hasa katika taaluma kujifunza na ujifunzaji wa wanafunzi.

"Tumeona fursa ambazo zipo katika matumizi ya akili unde, ikumbukwe kuwa wakati tunaanza kama nchi kulikuwa na hofu kwamba kazi zitapungua,fursa zitapungua na badala yake akili unde ndio itachukua nafasi za ajira kwa wahitimu wetu, lakini leo tumejifunza kuwa haiwezi kuchukua nafasi,lakini ni fursa kwa wahitimu wetu kuitumia katika kazi."
Aidha, amewasihi wanafunzi na wahitimu kutumia akili unde kwa kufuata weledi wakitambua kwamba bado wanahitaji kuchakata na kufikiria na kuendelea kupata maarifa na sio tu kuhamisha wanachokipata kule ila iwasaidie katika kuchakata taarifa zao.
"Na bado kuna kile kipengele cha akili ya mwanadamu katika kufikiri na kuchakata taarifa anazopata kitu kinahitaji umakini,"amesisitiza.
Kwa upande wake Mkufunzi katika Kongamano hilo, Dkt. Hellen Maziku amesema,matumizi ya akili unde yapo kila sehemu na ndio inatumika zaidi duniani,hata hivyo bado binadamu ana kazi ya kufikiri,kwa akili unde haifikiri kama yeye."Sasa tuna kazi ya kufikiri kwa sababu akili unde haiwezi kufikiri akili unde haiwezi kuchukua kazi za ustawi wa jamii,kazi hizi zinahusisha kwenye jamii na zinahusisha hisia zaidi ila akili unde itabadilisha namna ambayo unafanya kazi, kwani utatumia kwa mambo fulani.Ni lazima tubadilishe akili zetu kwani haiepukiki,"amesisitiza Dkt.Maziku.







