DAR-Bodi ya Bima ya Amana (DIB) ipo katika mchakato wa kulipa fidia ya ufilisi awamu ya tatu ya asilimia 30 kwa wadai wa iliyokuwa benki ya FBME walioko Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa DIB, Bw.Isack Kihwili.
Malipo haya yanafanya wadai wa FBME nchini wawe wamelipwa jumla ya asilimia 85 ya madai yao,kwani katika awamu ya kwanza na ya pili walilipwa asilimia 30 na asilimia 25, mtawalia.
‘’Kutokana na tathmini iliyofanywa, DIB imeamua kulipa fidia ya ufilisi kwa wadai waliokuwa na amana zaidi ya shilingi milioni 1,500,000.00 katika benki ya FBME kwa awamu ya tatu kwa upande wa wadai wa Tanzania pekee,’’ amesema Mkurugenzi Mkuu wa DIB, Bw. Isack Kihwili katika taarifa yake aliyoitoa leo Desemba 1,2025.
Aidha,Kamati ya Wadai imeshaidhinisha pendekezo la malipo hayo.Kwa ujumla, wadai kwa upande wa Tanzania ni 1,414, ambao madai yao ya jumla kwa benki hiyo ni shilingi bilioni 35.2; wadai wa kimataifa (TIB) wako 866 na madai yao ni shilingi bilioni 308.22.
Aidha,wateja wa tawi la Cyprus ni 5,480 wakidai jumla ya Euro milioni 1,254.62 (sawa na shilingi milioni 3,596.00).
‘’Malipo ya awamu nyingine yatategemea kiasi kitakachokusanywa ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa fedha zilizozuiliwa na mamlaka ya Marekani (FinCEN),’’ ameeleza Mkurugenzi Mkuu wa DIB na kuongeza kuwa kuzuiliwa kwa fedha hizo ni moja ya sababu kubwa zilizochelewesha mchakato wa malipo ya fidia ya ufilisi.
Aidha, DIB kama mfilisi, itaendelea kufanya tathmini kadiri makusanyo yatakavyopatikana na kufanya malipo ya awamu nyingine kwa wadai pindi yatakapokuwa ya kuridhisha.
Benki Kuu ya Tanzania ilifuta leseni ya Benki ya FBME mwaka 2017 kutokana na kukiuka masharti ya yake na kuichagua DIB kama Mfilisi.
FBME ilikuwa na makao makuu yake hapa nchini na tawi nchini Cyprus. Hii imefanya zoezi la ufilisi kushirikisha mamlaka za Tanzania na Cyprus.
Tags
Bodi ya Bima ya Amana (DIB)
Deposit Insurance Board
(DIB)
FBME BANK LIMITED
Habari
The Deposit Insurance Board (DIB)

Taarifa nzuri, isipokuwa kuna makosa machache ya kiuandishi na hasa katika kutaja viwango vya fedha.
ReplyDelete