Wateja wa iliyokuwa Benki ya FBME waanza kupokea asilimia 30 ya fidia

DAR-Baadhi ya wateja wa iliyokuwa FBME Bank Limited (iliyo katika ufilisi) wameanza kupokea fidia ya ufilisi ya asilimia 30 iliyotangazwa hivi karibuni na Bodi ya Bima ya Amana (DIB).
Wateja hao, wameeleza hayo katika ujumbe wao kwa DIB wakielezea furaha yao baada ya kupokea fedha zao kwenye akaunti zao.

“Asante sana. Hela zimeingia muda si mrefu hapa. Nashukuru. Leo nitakula vizuri,” ameeleza mteja mmoja wa iliyokuwa benki ya FBME huko Mwanza baada ya kupokea malipo ya awamu ya tatu ya asilimia 30 katika akaunti yake.

Aidha, mnufaika mwingine wa fidia hiyo ya ufilisi ameeleza shukurani zake kwa wote ambao wamewezesha na wanawezesha kupatikana kwa fedha hizo zinazotokana na kufutiwa leseni FBME kutokana na kukiuka masharti ya leseni na kuwekwa chini ya ufilisi.

“Mimi ninashukuru na ninawashukuru sana kwa msaada wao na yeyote anayehusika kutupambania katika suala hili,” amesema mnufaika mwingine katika ujumbe wake kwa DIB.

DIB ilitangaza mapema wiki hii kuanza kwa mchakato wa kulipa fidia ya ufilisi awamu ya tatu ya asilimia 30 kwa wadai wa iliyokuwa benki ya FBME walioko Tanzania.

Malipo haya yanafanya wadai wa FBME nchini wawe wamelipwa jumla ya asilimia 85 ya madai yao, kwani katika awamu mbili za kwanza walilipwa jumla ya asilimia 55.

‘’Kutokana na tathmini iliyofanywa, DIB imeamua kulipa fidia ya ufilisi kwa wadai waliokuwa na amana zaidi ya shilingi milioni 1,500,000.00 katika benki ya FBME kwa awamu ya tatu kwa upande wa wadai wa Tanzania pekee,’’ alieleza Mkurugenzi Mkuu wa DIB, Bw. Isack Kihwili wakati anatangaza kuanza kulipwa fidia ya awamu ya tatu.

Kwa ujumla, wadai kwa upande wa Tanzania ni 1,414, ambao madai yao ya jumla kwa benki hiyo ni shilingi bilioni 35.2; wadai wa kimataifa (TIB) wako 866 na madai yao ni shilingi bilioni 308.22. 

Aidha, wateja wa tawi la Cyprus ni 5,480 wakidai jumla ya Euro milioni 1,254.62 (sawa na shilingi milioni 3,596.00).

Malipo ya awamu nyingine yatategemea kiasi kitakachokusanywa ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa fedha zilizozuiliwa na mamlaka ya Marekani (FinCEN). Aidha, DIB kama mfilisi, itaendelea kufanya tathmini kadiri makusanyo yatakavyopatikana na kufanya malipo ya awamu nyingine kwa wadai pindi yatakapokuwa ya kuridhisha.

Benki Kuu ya Tanzania ilifuta leseni ya Benki ya FBME mwaka 2017 kutokana na kukiuka masharti ya leseni yake na kuichagua DIB kama Mfilisi. FBME ilikuwa na makao makuu yake hapa nchini na tawi nchini Cyprus. Hii imefanya zoezi la ufilisi kushirikisha mamlaka za Tanzania na Cyprus.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news