Waturuki wajifunza Kiswahili kwa kasi ya 5G

ANKARA-Desemba 23, 2035, Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari alifanya mazungumzo na ujumbe kutoka Kituo cha Mafunzo ya Kikanda (Regional Studies Center-BAM) kilichopo Ankara, Uturuki ambacho pamoja na mambo mengine kinajihusisha na kufundisha Lugha ya Kiswahili.
Ujumbe huo uliohusisha wanafunzi na waratibu wa kituo hicho uliongozwa na Dkt. Hursit Dingil na ulimweleza Balozi Bakari kuhusu majukumu ya Kituo hicho ambayo ni kutoa mafunzo ya masuala ya kikanda na lugha za kimataifa ikiwemo Kiswahili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Ulifafanua kuwa mafunzo ya Kiswahili wanayotoa katika Kituo cha BAM yanalenga kuwaandaa wataalamu kwa kuwapa ujuzi muhimu wa lugha utakaowasaidia katika mawasiliano, kufanya utafiti na kukuza uelewa wa utamaduni, historia na mienendo ya ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwemo nchi ya Tanzania.

Ujumbe huo ulishukuru ushirikiano unaopata kutoka Ubalozini katika kufundisha Kiswahili kwa kuwapatia mwalimu na vitabu vya kujifunzia Kiswahili.

Wamebainisha kuwa wanafunzi wao tayari wameweza kuandika na kuzungumza Kiswahili, jambo ambalo limeonesha mafanikio ya mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Balozi Bakari amekipongeza kituo hicho kwa uamuzi wa busara wa kujumuisha Kiswahili kwenye mafunzo ya lugha yanayotolewa kituoni hapo.

Amebainisha kwamba Ubalozi utaendelea kutangaza lugha ya Kiswahili nchini Uturuki kama sehemu ya kubidhaisha lugha hiyo adhimu duniani ambayo inatambuliwa kimataifa.
Aidha, amewahakikishia wanafunzi hao utayari wa Ubalozi kushirikiana na kituo hicho ili kuendeleza programu za mafunzo ya Kiswahili kwa wanafunzi zaidi wenye nia hiyo.

Vilevile, amesema kwamba programu ina mchango chanya katika kudumisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Uturuki na kutumika kama daraja la kitamaduni linalokuza maelewano na mshikamano baina ya nchi hizi mbili.

Hicho ni kituo cha pili kinachotoa mafunzo ya Kiswahili nchini Uturuki ambacho kinasimamiwa na Ubalozi kikiwemo kituo kingine kilichopo jijini Istanbul. Ubalozi umekusudia kuendeleza jitihada za kufundisha Kiswahili kwa kufungua vituo zaidi pamoja na kutafuta wadau wa kushirikiana nao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news