ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025–2030, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar pamoja na sera na miongozo mbalimbali, inaendelea kuboresha mazingira ya utoaji na upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote.
Akizungumza katika Mahafali ya 13 ya Zanzibar School of Health yaliyofanyika katika Uwanja wa Mao Zedong, Wilaya ya Mjini Unguja, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya afya, ikiwemo upatikanaji wa dawa, vifaa tiba pamoja na kuboresha maslahi ya watumishi ili kuongeza ari katika utendaji wao.
Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imepanga kuajiri watumishi 1,566 wa Sekta ya Afya ili kuongeza kasi ya utoaji wa huduma mijini na vijijini.
Aidha, amesema Serikali imeongeza ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka 8,870 mwaka 2024 hadi kufikia wanafunzi 20,000, hatua ambayo inalenga kuwawezesha vijana kujiendeleza na kufikia ngazi za juu za ubingwa na ubobezi katika kada mbalimbali za afya.Mhe. Hemed amewataka wahitimu hao kujenga utayari wa kiutumishi, kushirikiana na wenzao katika kufanikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, sambamba na kuzingatia uadilifu, huruma, heshima na misingi ya taaluma yao ili kuepusha vitendo vinavyoweza kuidhalilisha sekta ya afya.
Ameupongeza uongozi wa Zanzibar School of Health kwa juhudi zake za kuimarisha ubora wa elimu na kuendelea kuanzisha kozi muhimu ikiwemo kozi mpya ya Maabara. Amewataka kuendeleza tafiti, kuwaendeleza kielimu watumishi waliopo kazini na kubuni mitaala inayokidhi mahitaji ya Taifa.
Makamu wa Pili wa Rais amet reaffirm kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa chuo hicho na vyuo vingine nchini ili viendelee kuzalisha wataalamu waliobobea watakaolitumikia Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohamed Mussa, amesema wizara yake itaendelea kushirikiana na uongozi wa Zanzibar School of Health ili kuhakikisha chuo hicho kinaendelea kutoa taaluma bora za afya.






