DODOMA-Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Crispin Chalamila, Januari 19, 2026, ametoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu majukumu, mamlaka na muundo wa Taasisi hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete.
Taarifa hiyo ilitolewa jijini Dodoma ikilenga kuijengea uwezo kamati hiyo ambayo ni mpya baada ya kuundwa katika Bunge la 13, ili iweze kutekeleza majukumu yake ya usimamizi wa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais kwa ufanisi.Akizungumza wakati wa wasilisho lake, Bw. Chalamila alibainisha kuwa,majukumu makuu ya TAKUKURU ni pamoja na kuzuia rushwa, kuchunguza vitendo vya rushwa, kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya rushwa, pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali juu ya mifumo na taratibu zinazoweza kuondoa mianya ya rushwa katika sekta za umma na binafsi.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu huyo alielezea muundo wa TAKUKURU kuanzia Makao Makuu, Ofisi za Mikoa, Wilaya pamoja na vituo maalum.
Baada ya wasilisho hilo, baadhi ya Wajumbe wa Kamati waliuliza maswali na kutoa ushauri mbalimbali wa namna ya kuimarisha utendaji wake.
Pamoja na mambo mengine, wajumbe wa kamati walisisitiza umuhimu wa TAKUKURU kufuatilia miradi ya maendeleo katika hatua zote za utekelezaji ili kuhakikisha inatekelezwa kwa thamani halisi ya fedha na kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.
Vilevile, Kamati ilitoa maoni kuhusu umuhimu wa kulindwa kwa watoa taarifa na mashahidi, ikisisitiza kuwa ulinzi wa kisheria kwa watoa taarifa ni nyenzo muhimu katika kuimarisha mapambano dhidi ya Rushwa.
Akihitimisha wasilisho hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, aliwahakikishia Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati kuwa maelekezo, ushauri na mapendekezo ya kamati yatazingatiwa, kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa TAKUKURU na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa nchini.