NKASI-Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. James Kilabuko amezindua nyaraka za usimamizi wa maafa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa huku akisisistiza nyaraka hizo kutekelezwa kwa vitendo.

Dkt. Kilabuko amesema hayo leo 27 Januari, 2026 wakati wa uzinduzi huo na kusema kuwa, hatua hiyo ni mwanzo wa kuanza kazi rasmi endapo kutatokea janga lolote, na kutoa wito kwa idara, vitengo na taasisi ngazi ya wilaya kuzingatia nyaraka hizo kwa kuhakikisha zinakuwa chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau katika masuala ya menejimenti ya maafa.
Ameongeza kuwa, hatua hiyo itasaidia kujenga uelewa wa jamii kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa, kuimarisha mfumo wa utoaji wa tahadhari awali, kujenga uwezo wa kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.
Dkt. Kilabuko alifafanua kuwa, nyaraka hizo zimekuja wakati sahihi kwa kuzingatia kuwa, Wilaya imekuwa ikikabiliwa na maafa yanayosababishwa na majanga hasa ya upepo mkali, magonjwa ya mlipuko kwa binadamu na wanyama, mafuriko pamoja na mgongano wa wanyamapori na binadamu ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara.
"Nimeelezwa kuwa matokeo ya tathmini ya maafa iliyofanyika katika Halmashauri ya Nkasi mwezi Januari, 2026 yalionesha kuwa yapo majanga mengine ambayo yamekuwa yakijitokeza japo hayajaleta athari kubwa ikiwemo wadudu waharibifu wa mazao, ajali za barabarani, moto, ajali za majini, tetemeko la ardhi, radi pamoja na maporomoko ya ardhi.
"Natambua kuwa Wilaya imekuwa ikikabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, nitumie fursa hii kuwapongeza kwa jitihada mnazoendelea nazo katika kukabiliana na ugonjwa huo,”amesema Dkt. Kilabuko.
Kwa hatua nyingine, ameshukuru Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kwa ufadhili ambao umewezesha kuchangia jitihada za Serikali katika kuandaa Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa pamoja na Mkakati wa Kupunguza Vihatarishi vya Maafa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Naye Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Brigedia Generali Hosea Ndagala amesema Idara hiyo imekuwa ikichukua hatua za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Aliongezea kuwa,Serikali kwa kutambua hilo na katika kuhakikisha nchi inakuwa stahimilivu dhidi ya maafa, imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali.
Jitihada hizo ni pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kushughulikia masuala ya maafa kwa kutunga Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004, Toleo la Mwaka 2025 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Sura ya 242 ambayo imeweka mfumo mzuri wa usimamizi wa maafa kutoka ngazi ya Taifa hadi Kijiji/Mtaa.
“Ni muhimu kwa Halmashauri kuendelea kutenga fedha katika bajeti juu ya utekelezaji wa Mpango huu uliozinduliwa leo na kuendelea kutoa elimu kuhusu namna bora ya wananchi kuendelea kuchua hatua za awali kwa kuzingatia maafa ni suala mtambuka na linaanza na mtu mmoja,” alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mheshimiwa Peter Lijualikali ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu na UNICEF kwa kazi nzuri ya uandaaji wa nyaraka za usimamizi wa maafa na kutoa elimu juu ya masuala ya menejimenti ya maafa kwa Wilaya ya Nkasi na kuahidi kuzifanyia kazi nyaraka hizo.“Wilaya imepata kitu chema kitakachotufaa, nasi tunaahidi kuzitumia kama miongozo sahihi ya kuleta matokeo kwa kuzingatia Serikali imeweka fedha katika kuhakikisha mipango inaleta matokeo yaliyokusudiwa, hivyo tusiwe nyuma, tufanyie kazi kwa tija ya Halmashauri nzima,” alisema Lijualikali
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Nkasi Mheshimiwa Richard Leonard Masai akitoa Salam ameshukuru uratibu mzuri wa uandaaji wa nyaraka hizo na kutoa rai kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhali za awali na kuzingatia taarifa za tahadhali zinazotolewa na wataalamu ili kuendeala kuwa na jamii iliyo salama na yenye kujiletea maendeleo yake.






