NA DIRAMAKINI
MCHEZAJI wa Klabu ya Young Africans Sports Club (Yanga SC), Duke Abuya ametangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Disemba wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026, huku Pedro Goncalves wa klabu hiyo hiyo akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 23,2025 na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Abuya alionesha kiwango cha juu katika michezo miwili aliyocheza mwezi Disemba, akiisaidia Young Africans kuibuka na ushindi katika mechi zote hizo pamoja na kufunga mabao mawili ndani ya dakika 180 za mchezo. Ushindi huo uliipa timu yake pointi muhimu katika mbio za ubingwa.
Katika mchakato wa tuzo hizo, Abuya aliwashinda Nassor Saadun wa Azam FC na Prince Dube wa Young Africans, walioingia naye fainali katika mchakato wa upigaji kura uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Vilevile kwa upande wa kocha, Pedro Goncalves aliwashinda Florent Ibenge wa Azam FC na Etienne Ndayiragije wa TRA United.
Young Africans chini ya Goncalves ilishinda mechi zote mbili ilizocheza mwezi huo, ikiifunga Fountain Gate kwa mabao 2-0 na Coastal Union kwa bao 1-0, na kupanda kutoka nafasi ya nne hadi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Wakati huo huo, Said Mpoche, Meneja wa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, alichaguliwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa Mwezi Disemba kutokana na usimamizi mzuri wa michezo pamoja na miundombinu ya uwanja huo.
Katika Ligi ya Championship ya NBC, mchezaji wa Transit Camp, Adam Uledi, alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Disemba, huku Shadrack Nsajigwa wa klabu hiyo hiyo akitangazwa kuwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Uledi aliingia fainali pamoja na Obrey Chirwa wa Kagera Sugar na Boniface Mwanjonde wa Mbeya Kwanza, akionesha kiwango bora katika michezo mitano aliyocheza kwa dakika 450.
Aidha,Nsajigwa aliwashinda Juma Kaseja wa Kagera Sugar na Zuberi Katwila wa Geita Gold baada ya kuiongoza Transit Camp kushinda mechi zote tano za mwezi Disemba.
