DODOMA-Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar, amekutana na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. Andrew Lentz, katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma kwa mazungumzo kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Marekani.
Mazungumzo hayo yalilenga zaidi kujadili fursa za kukuza uwekezaji, kuboresha mazingira ya biashara na kuendeleza sekta muhimu zinazochochea ukuaji wa uchumi, zikiwemo teknolojia ya kidijitali, kilimo, dawa, na uzalishaji wa viwandani.
Katika kikao hicho, Mhe. Lentz alibainisha kuwa kampuni nyingi za Kimarekani ziko tayari kushirikiana na kampuni za Kitanzania katika mikataba yenye manufaa kwa pande zote, hususan katika miradi inayochangia ajira na maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha alielezea juhudi za Serikali katika kuendelea kuboresha mfumo wa kodi, taratibu za uwekezaji, na kuimarisha miundombinu ili kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi nchini.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Kamisha wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Melkizedeck Mbise, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Madeni, Wizara ya Fedha, Bw. Omary Khama, Mshauri wa Masuala ya Ulinzi wa Ubalozi wa Marekani, Luteni Kanali Michael Kummererna, maafisa wengine wa Wizara ya Fedha.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani ulianzishwa rasmi mwaka 1961, mara baada ya Tanganyika kupata uhuru. Kwa zaidi ya miongo sita, nchi hizi zimekuwa washirika wa karibu katika nyanja mbalimbali ikiwemo maendeleo ya kijamii, elimu, afya, na utawala bora.Kupitia uhusiano huo uliojengeka kwa misingi ya urafiki na heshima, Tanzania na Marekani zinaendelea kuimarisha ushirikiano unaolenga manufaa ya pamoja.




