Dunia ya Marekani


DUNIA ni ya Marekani? Katika siasa za Kimataifa, swali hili limekuwa likiibua hoja nyingi bila majibu kamili, huku wengine wakiishia kuelezea ukubwa na ushawishi wa taifa hilo kuliko mataifa mengine.
Kauli hii haimaanishi umiliki wa kisheria, bali inaonesha namna nguvu za kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia za Marekani zinavyoathiri maamuzi ya nchi huru.

Venezuela ni mfano unaoonesha hali hii kwa uwazi na tayari imevamiwa na Rais Maduro inasemekana hayupo nchini.

Kwa miaka kadhaa, Marekani imekuwa ikishinikiza Venezuela kupitia vikwazo vya kiuchumi na hatua za kidiplomasia, ikisisitiza kulinda demokrasia.

Hata hivyo, hatua hizi zimetafsiriwa na wakosoaji kama uingiliaji wa masuala ya ndani, hasa pale Marekani ilipojitokeza kuunga mkono uongozi mbadala wa kisiasa.

Nguvu ya dola ya Marekani katika mfumo wa fedha wa Dunia, pamoja na ushawishi wake katika taasisi za kimataifa, huifanya iweze kuathiri uchumi na maisha ya wananchi wa mataifa mengine bila uvamizi wa kijeshi.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabaki na swali la msingi kuwa,uhuru wa mataifa madogo una nafasi gani katika mfumo wa dunia unaotawaliwa na nguvu za wakubwa kama Marekani?.

Kwa msingi huo, Venezuela inabaki kuwa kielelezo cha changamoto ya usawa na haki katika uongozi wa dunia. Endelea;

1. Dunia ya Marekani, wala hii siyo yetu,
Angani na hata chini, hatuna amri zetu,
Kwao siyo uhaini, nchi huru siyo kitu,
Ya kwamba Venezuela, inavurugwavurugwa.

2. Alianza taratibu, Trump mbabe wetu,
Kumbe mengi aratibu, ya kuwabana wenzetu,
Licha ya zile adhabu, za kuua ua watu,
Ya kwamba Venezuela, inavurugwavurugwa.

3. Ilipiga baharini, huko ikaua watu,
Kiwatia hatiani, waleta uraibu tu,
Majini hata angani, ikawa Marekani tu,
Ya kwamba Venezuela, inavurugwavurugwa.

4. Maduro yule Rais, sasa hayuko na watu,
Waliompa nafasi, awe ni kiongozi tu,
Yeye kama karatasi, kadakwa kitenesi tu,
Ya kwamba Venezuela, inavurugwavurugwa.

5. Hii si mara ya kwanza, katika dunia yetu,
Marekani lishaanza, kuwadakadaka watu,
Wale waliojiponza, kuiona siyo kitu,
Ya kwamba Venezuela, inavurugwavurugwa.

6. Likuwepo Noriega, mbabe kati ya watu,
Yeye zake zote swaga, walimkamata watu,
Na kesi wakaipiga, akawa ni mfungwa tu,
Ya kwamba Venezuela, inavurugwavurugwa.

7. Ya Osama bin Laden, alitisha yule mtu,
Wakafanya Marekani, kuutoa wake utu,
Si kwao Pakistani, wakafanya vyao vitu,
Ya kwamba Venezuela, inavurugwavurugwa.

8. Naye Saddam Hussein, Kanali Gaddafi watu,
Wote walipigwa chini, mbinu ni hizi za watu,
Kweli hapa duniani, ni kama Marekani tu,
Ya kwamba Venezuela, inavurugwavurugwa.

9. Kwamba ni demokrasia, hiyo wala siyo kitu,
Mbabe ajifanyia, bila ya kujali kitu,
Malengo akifikia, ni demokrasia ya kwetu,
Ya kwamba Venezuela, inavurugwavurugwa.

10. Dunia ya Marekani, tujitambue mwakwetu,
Na macho tuweke chini, tusijejifanya fyatu,
Tuingie msambweni, tubakie bila kitu,
Ya kwamba Venezuela, inavurugwavurugwa.

11. Chote tutakacho fanya, akili kichwani mwetu,
Marekani akiminya, tujue hatuna chetu,
Alionya anaonya, tufyate mikia yetu,
Ya kwamba Venezuela, inavurugwavurugwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here