NA MARY GWERA,
Mahakama
CHAMA cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) kimeandika historia kwa kufanya Bonanza la Michezo la aina yake jijini Dodoma ambapo Mahakama za Kanda ya Ziwa na Magharibi zilimaliza mashindano hayo kwa shangwe, vifijo na nderemo baada ya kuibuka kidedea katika michezo mbalimbali ikiwemo wa Mpira wa Miguu.


Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akipiga mpira kuashiria ufunguzi wa Bonanza la Michezo la Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) kwa kuanza kuchezesha mchezo wa Mpira wa Miguu kati ya Timu ya Mpira wa Miguu ya Kanda ya Kati na ya Kanda ya Ziwa na Magharibi uliofanyika katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma.
Akifungua Bonanza hilo mapema jana tarehe 16 Januari, 2026 katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma, Mgeni Rasmi ambaye alikuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju alitoa rai kwa Wanachama wa Chama hicho na watumishi wa Mahakama kwa ujumla kuendeleza utaratibu wa kushiriki katika michezo mbalimbali sambamba na kufanya mazoezi ili kujiepusha na magonjwa ikiwemo Kisukari, Shinikizo la Damu na mengine.
Ufunguzi wa Bonanza hilo la Michezo ulifanyika kuanzia saa 3 Asubuhi ambapo Mhe. Masaju alishiriki kwa kuanza kuchezesha Kabumbu kati ya Timu ya Mpira wa Miguu ya Kanda ya Kati na ya Kanda ya Ziwa na Magharibi.
Mbali na Mpira wa Miguu, michezo mingine iliyohusika katika Bonanza hilo ni pamoja na Mpira wa pete, Riadha mita 100, Kuvuta Kamba, Kukimbia kwenye gunia, Kukimbiza kuku, Kuendesha Baiskeli, Karata, Drafti, Mchezo wa Bao, (Pool table), Rede, (Dancing Chair) na Kukimbia na yai kwenye kijiko.
Aidha, Bonanza hilo lilishirikisha Wadau wengine wa Mahakama ikiwa ni pamoja na Mawakili wa Serikali, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Madini na Watumishi wasiokuwa wanachama TMJA (Non-Judicial officers).
Kuhusu matokeo ya michezo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ambaye ni Mratibu wa matokeo ya michezo, Mhe. Arnold Kirekiano alitangaza washindi katika michezo yote ambapo alieleza kuwa, washindi walipewa Vikombe na Medali.
“Washindi kwa baadhi ya michezo Mpira wa miguu Mshindi wa kwanza ni Kanda ya Ziwa na Magharibi, Mshindi wa pilli Kanda ya Kati,” alisema Mhe. Kirekiano.
Kwa upande wa Mpira wa pete, Jaji Kirekiano amesema kuwa, mshindi wa kwanza ni Kanda ya Kati, Mshindi wa pili Kanda ya Ziwa na Magharibi na Kuvuta Kamba wanaume mshindi wa kwanza ni Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Mshindi wa pili ni Kanda ya Ziwa na Magharibi, Kamba wanawake mshindi wa kwanza ni Kanda ya Nyanda Za Juu Kusini na Mshindi wa pili ni Kanda ya Kati.
Akizungumzia shindano la wadau, Mratibu huyo alisema kuwa, Mawakili wa Serikali wanaume na wanawake waliwashinda wenzao wa Magereza katika mchezo wa Kuvuta Kamba.
Aidha, Jaji Kirekiano alisema, michezo yote ilisimamiwa na waamuzi wenye taalamu na wazoefu ili kuweza kuboresha ufanisi, kutenda haki na usawa.
Aliongeza kuwa, zawadi zilizoandaliwa kwa washindi wa michezo ni tuzo za vikombe pamoja na medali.
Akizungumzia kuhusu mgawanyo wa Timu, Mhe. Kirekiano alisema Time ziligawanywa katika makundi manne ambapo Kanda ya Ziwa na Magharibi ilihusisha Musoma, Mwanza, Bukoba, Tabora, Kigoma, Geita, Simiyu na Shinyanga.
Alisema Timu nyingine ilikuwa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ilihusisha Iringa, Mbeya, Ruvuma, Songwe, Sumbawanga, Njombe na Katavi.
Timu nyingine ilikuwa ya Kanda ya Kaskazini na Pwani iliyohusisha mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Arusha na Tanga.
“Timu nyingine ni ya Kanda ya Kati inayohusisha Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu Masjala Kuu, Dodoma, Manyara na Singida,” alisema.
Kufanyika kwa Bonanza hilo kumehitimisha mtiririko wa matukio mbalimbali ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) uliofunguliwa tarehe 13 Januari, 2026 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kufungwa tarehe 16 Januari, 2026 na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju.
Zifuatazo ni picha mbalimbali za matukio-Bonanza la Michezo la Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) lililofanyika jana tarehe 16 Januari, 2026 katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akiwasalimia na kuwatakia kila la kheri Wanakabumbu kutoka Timu ya
Timu ya Mpira wa Miguu ya Kanda ya Kati na ya Kanda ya Ziwa na Magharibi zilizocheza jana tarehe 16 Januari, 2026 katika Bonanza la Michezo lililoandaliwa na Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) na kufanyika katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Bonanza la Michezo la Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) tarehe 16 Januari, 2026 katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma. Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Maandalizi ya Bonanza la TMJA, Mhe. Shaaban Lila na kulia ni Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), Mhe. Elimo Massawe.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Bonanza la Michezo la Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) tarehe 16 Januari, 2026 katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma. Kulia kwa Jaji Mkuu ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija na anayefuata ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Maandalizi ya Bonanza la TMJA, Mhe. Shaaban Lila.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Maandalizi ya Bonanza la TMJA, Mhe. Shaaban Lila akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Bonanza la Michezo la Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) tarehe 16 Januari, 2026 katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania akiongoza pamoja na Wanachama wengine wa TMJA, Watumishi wa Mahakama na Wadau wakiwa katika mazoezi ya kupasha viungo kabla ya kuanza kwa michezo mbalimbali iliyoandaliwa katika Bonanza hilo lililofanyika jana tarehe 16 Januari, 2026 katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma.
Shangwe kama lote baada ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya kuongoza Wanakabumbu wenzake kupokea Kombe baada ya Timu ya Mpira wa Miguu kutoka Kanda ya Ziwa na Maghariki kuibuka Mshindi katika mchezo huo uliofanyika tarehe 16 Januari, 2026 katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dar es Salaam.
Wana Kanda ya Ziwa na Magharibi wakifurahia ushindi mara baada ya kupokea Kombe la Mshindi wa jumla wa Bonanza la Michezo lililoandaliwa na Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA)
Majaji Wafawidhi na sehemu ya Majaji wengine kutoka Mahakama Kanda ya Ziwa na Magharibi wakifurahia ushindi wa ujumla waliopata katika mashindano ya michezo ya Bonanza yaliyofanyika katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma.
Wataalamu wa Mchezo wa bao wakiwa katika anga yao..
Wanabaiskeli.
Ni mwendo kwa mwendo na mbio kwa mbio mpaka kuku akamatwe na mshindi apatikane.
Wana Netiboli nao hawakuwa nyuma.
Watu Kazi wakiwa kazini, ilikuwa ni vuta nikuvute yaani mpaka kieleweke.
Mashabiki nao hawakuwa nyuma.



















