NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Mkoa wa Geita limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi kwa kufanya operesheni, misako na doria mbalimbali zilizozaa matokeo chanya, ambapo jumla ya watuhumiwa 200 wamekamatwa kwa tuhuma za makosa mbalimbali ya jinai.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,SACP Safia Jongo amesema kuwa, kuanzia Januari 1 hadi 17, 2026, watuhumiwa hao wamekamatwa kwa makosa yakiwemo kumiliki noti bandia, kuiba mali za wizi na kuingia nchini bila vibali halali.
Makosa mengine ni kumiliki nyara za Serikali, kuuza na kutengeneza pombe haramu ya moshi (gongo) pamoja na kumiliki vifaa vya ramli chonganishi.
Katika operesheni iliyofanyika Januari 5, 2026 majira ya saa 5 usiku,SACP Safia Jongo amesema, polisi walipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu mtu anayehusishwa na noti bandia katika Mtaa wa Mwatulole, Kata ya Buhalahala, Manispaa ya Geita.
Amesema, kufuatia taarifa hiyo, Polisi walifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Lavio Edgar akiwa ndani ya gari aina ya Harrier rangi ya silver lenye namba ya chassis ACU300018478.
SACP Safia Jongo amesema,upekuzi uliofanywa ulimbaini mtuhumiwa huyo akiwa na noti bandia za Kitanzania zenye thamani ya shilingi 1,931,000/= pamoja na vifaa vilivyotumika kutengenezea noti hizo, vikiwemo tarakilishi aina ya HP (Desktop) na printa aina ya Epson L3110. Aidha, alikutwa pia na nyaraka mbalimbali za Serikali zilizoghushiwa.
Katika ufuatiliaji ulioendelea hadi mikoa jirani, Polisi waliwakamata watuhumiwa wengine wawili, akiwemo Christian Christopher aliyekutwa na noti bandia zenye thamani ya shilingi 26,000/= na Upendo Emanuel aliyekutwa na noti bandia zenye thamani ya shilingi 473,000/=. Hivyo, jumla ya noti bandia zilizokamatwa zina thamani ya shilingi 2,430,000/=.
Katika hatua nyingine,amesema polisi waliwakamata watuhumiwa 47 kwa tuhuma za wizi wa mali mbalimbali zikiwemo pikipiki 41, ng’ombe 8, mbuzi 73, mabati 5, magodoro 5, friji 1, sofa 4, zulia 1 na subwoofer 1. Baada ya taratibu za kisheria, mali hizo zimerudishwa kwa wamiliki wake halali.
Pia, watuhumiwa 26 walikamatwa wakihusishwa na pombe haramu ya moshi (gongo), ambapo jumla ya lita 177 za pombe hiyo pamoja na mitambo yake ya utengenezaji zilinaswa.
SACP Safia Jongo amesema,Jeshi la Polisi pia liliwakamata watuhumiwa wawili waliokuwa wakimiliki nyara za Serikali, ambazo ni ngozi ya simba mmoja na ngozi ya chui mmoja.
Aidha, watuhumiwa 21 walikamatwa kwa kuingia nchini bila kibali halali, huku mtuhumiwa mmoja akikamatwa akiwa na vifaa vya ramli chonganishi.
Watuhumiwa wote wanaendelea kushikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi, kabla ya kufikishwa mahakamani.
Jeshi la Polisi limesema linaendelea kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali kubaini mtandao mzima wa wahalifu wanaohusika na matukio hayo.
Vilevile, Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limetoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu kwa wakati, huku likiahidi kuendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaohatarisha usalama wa wananchi na mali zao.
