NA GODFREY NNKO
SERIKALI imesema kuwa, uwekezaji uliofanywa na DP World pamoja na TEAGTL kupitia utaratibu wa ukodishaji na uendeshaji wa bandari nchini umeleta mafanikio makubwa.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw.Gerson Msigwa ameyasema hayo leo Januari 20,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali nchini katika Bandari ya Dar es Salaam jijini Dar es Salaam.
Msigwa amesema, kuna ongezeko la shehena hadi kufikia tani milioni 27.7 katika mwaka wa fedha 2024/2025 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na tani milioni 23.69 za shehena zilizohudumiwa mwaka 2023/2024 wakati wawekezaji hao wanaanza kazi.
"Katika kipindi cha miezi sita kinachoanza mwezi Julai hadi Disemba, 2025 Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia jumla ya tani milioni 16.7 ambazo ni kubwa kwa asilimia 30 ukilinganisha na tani milioni 12.8 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho cha mwaka 2024.
Pia, Msigwa amefafanua kuwa, muda wa meli kuhudumiwa bandarini umepungua kutoka
wastani wa siku 30 hadi kufikia wastani wa siku 6 kwa meli za makasha ikijumuisha muda wa kusubiri nangani.
Katika hatua nyingine, Msigwa amefafanua kuwa,uwekezaji huo umetoa ajira ambapo hadi kufikia mwezi Juni 2025, jumla ya wafanyakazi 764 walipata ajira za moja kwa moja katika Kampuni za DP World na TEAGTL katika fani
mbalimbali.
Miongoni mwao ni Maafisa wa Idara mbalimbali, Makarani wa shughuli za uendeshaji, waendesha mitambo mikubwa na
midogo na askari.
Aidha mbali na ajira hizo za moja kwa moja,
Kampuni ya DP World na TEAGTL zimetengeneza pia ajira nyingine zisizo za moja kwa moja kufuatia ongezeko la shehena
mchanganyiko na shehena ya makasha.
"Ajira hizi zinajumuisha wafanyakazi wa kutwa, madereva wa malori, mawakala wa forodha na nyinginezo.
"Uwekezaji huu umeiwezesha pia TPA kupunguza kwa mafanikio makubwa gharama za uendeshaji hususani katika Bandari ya Dar es Salaam kwa wastani wa asilimia 57 kufuatia ushirikishaji wa DP World na TEAGTL katika utekelezaji na uendeshaji wa shughuli za bandari.
Msigwa amesema, hali hii imeimarisha uwiano wa faida kwa TPA kutoka wastani wa asilimia 66 hadi kufikia wastani wa asilimia 78.
Amesema, mafanikio mengine ni kuimarika kwa ufanisi na uendeshaji wa shughuli za Bandari ya Dar es Salaam, ambapo kumechangia pia kuongezeka kwa makusanyo ya mapato ya Serikali hususani yale yanayotokana na kodi ya forodha hadi kufikia Shilingi Trilioni 12.33 katika kipindi cha mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 17 ukilinganisha na makusanyo ya shilingi Trilioni 10.55 yaliyokusanywa katika kipindi cha mwaka 2023/24.
"Idadi ya abiria waliohudumiwa katika Bandari za TPA imekua ikiongezeka kutoka abiria 3,258,718 mwaka 2020/21 hadi abiria 4,050,740 mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 7 kwa mwaka."
