SIMIYU-Wakazi wa Mkoa wa Simiyu wamehimizwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati safi na salama ya kupikia.
Rai hiyo imetolewa leo Januari 29,2026 na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha wakati wa upokeaji wa mradi wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku mkoani hapo."Kinachofanyika leo ni kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan za upatikanaji na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia katika kutunza na kuhifadhi mazingira," alisema Mhe. Macha.
Mradi huu unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ni muendelezo wa juhudi za serikali katika kutunza mazingira na kuboresha afya za wananchi kwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia aliendelea kwa kusema, Mhe. macha.
Akizungumza wakati wa utoaji wa taarifa ya mradi, Mhandisi Mwandamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA),Deusdedith Malulu amesema,wakati taifa likiwa kwenye mkakati wa kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati safi na salama ya kupikia, Wakala wa Nishati Vijijini umekuja na mpango wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku yanayotumia kuni na mkaa mchache sana na yenye ufanisi mkubwa katika matumizi yake.
Aidha, mradi huu una lengo la kuimarisha na kuboresha afya za wananchi, mazingira, kukuza upatikanaji wa Nishati Safi na endelevu, kupanua usambazaji wa nishati mbadala katika maeneo ya Vijijini na zaidi kuhamasisha matumizi ya teknolojia safi kupitia teknolojia za kisasa na bora za kupikia.
Aidha, mradi huu wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wenye dhima mpaka ifikapo 2034 asilimia themanini (80%) ya watanzania wawe wanatumia nishati safi na salama ya kupikia.
Aidha, mkataba wa mradi huu ulisainiwa tarehe 09 Mei, 2025 kati ya REA na mtoa huduma kampuni ya Geita Millenium Star Company Limited na utatekelezwa kwa miezi 15 ambapo mtoa huduma atasambaza na kuuza majiko banifu 1,247 kwa bei ya ruzuku katika wilaya nne za mkoa wa Simiyu ambazo ni Itilima, Maswa, Busega na Meatu na majiko banifu 1,248 katika wilaya ya Bariadi.
Mhandisi Malulu amesema, gharama ya mradi ni kiasi cha zaidi ya TZS Milioni 257.5 ambapo serikali itatoa ruzuku ya zaidi ya TZS Milioni 218.9 na kufanikisha uuzaji na usambazaji wa majiko banifu 6,236.Aidha, jiko moja huwa linauzwa kwa kiasi cha TZS 41,300 lakini serikali itatoa ruzuku ya asilimia themanini na tano (85%) ambayo ni sawa na TZS 35,105 na hivyo mwananchi atanunua jiko kwa gharama ya TZS 6,195 tu.







