NA DIRAMAKINI
UONGOZI wa klabu ya Manchester United umefikia makubaliano ya kusitisha mkataba wa ajira wa kocha mkuu, Ruben Amorim kupitia uamuzi uliotangazwa rasmi asubuhi ya leo Januari 5,2026.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa klabu kurekebisha mwelekeo wa kiufundi kufuatia mwenendo usioridhisha wa matokeo.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo yenye maskani yake Old Trafford, Amorim ataondoka mara moja, huku Darren Fletcher akitarajiwa kuiongoza timu kama kocha wa mpito wakati klabu ikiendelea na mchakato wa kumtafuta kocha wa kudumu.
Amorim alichukua mikoba ya kuinoa Manchester United kwa matarajio makubwa, lakini kipindi chake hakikuweza kuleta uthabiti uliotarajiwa.
Katika jumla ya mechi 63 alizoiongoza, kocha huyo alishinda mechi 25, akapata sare 15 na kupoteza mechi 23 ikiwa ni rekodi ambayo haikuakisi malengo ya klabu hiyo yenye historia kubwa katika soka la England na Ulaya.
Wachambuzi wa soka wanaeleza kuwa, changamoto kubwa katika kipindi cha Amorim ilikuwa ni kushindwa kudumisha matokeo chanya mfululizo, hususan katika michezo muhimu ya ligi na mashindano ya kimataifa.
Hali hiyo ilisababisha presha kubwa kutoka kwa mashabiki na wadau wa klabu, waliokuwa wakitaka kuona mabadiliko ya haraka ndani ya benchi la ufundi.
Uongozi wa Manchester United umeeleza kuwa, uamuzi wa kufanya mabadiliko ya kiufundi umefikiwa baada ya tathmini ya kina, ukizingatia maslahi ya muda mfupi na mrefu ya timu.
“Klabu inaamini mabadiliko haya ni muhimu katika kuleta msukumo mpya na kuboresha matokeo uwanjani,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Darren Fletcher, ambaye ni mchezaji wa zamani wa klabu hiyo na amekuwa sehemu ya benchi la ufundi, anaingia katika nafasi ya mpito huku akitarajiwa kuhakikisha timu inapata utulivu wakati huu wa mpito.
Uzoefu wake ndani ya klabu unaonekana kuwa nyenzo muhimu katika kuendeleza mshikamano wa wachezaji na falsafa ya Manchester United.
Aidha, hatua hii inaifungua ukurasa mpya kwa klabu hiyo, huku macho ya mashabiki yakielekezwa kwenye uamuzi wa nani atakabidhiwa jukumu la kudumu la kuiongoza timu kuelekea mafanikio yanayolingana na hadhi ya Manchester United.
