NA DIRAMAKINI
TIMU ya Taifa ya Morocco imefanikiwa kufuzu hatua ya fainali ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Ni baada ya kuibuka na ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Nigeria katika mchezo mkali uliochezwa hadi dakika 120 bila mshindi.
Mtanange huo umepigwa Januari 14,2025 katika dimba la Prince Moulay Abdellah Stadium lililopo jijini Rabat nchini Morocco.
Aidha,mchezo huo wa nusu fainali, uliovuta hisia za mashabiki wengi wa soka barani Afrika, ulishuhudia timu zote zikionesha kiwango cha juu cha ushindani,lakini zikashindwa kupata bao ndani ya dakika 90 za kawaida pamoja na dakika 30 za nyongeza, hali iliyopelekea mshindi kupatikana kupitia mikwaju ya penalti.
Katika hatua ya penalti, Morocco ilionesha utulivu na umakini mkubwa, ambapo wachezaji wake walifanikiwa kutekeleza penalti nne kati ya tano, huku Nigeria ikifunga penalti mbili pekee, jambo lililowapa Morocco tiketi ya kucheza fainali ya mashindano hayo makubwa barani Afrika.
Ushindi huo unaifanya Morocco kuendelea kudhihirisha ukuaji wake katika soka la Afrika, huku ikionesha nidhamu ya kiufundi, uimara wa safu ya ulinzi na uwezo wa kustahimili presha katika michezo mikubwa.
Kwa upande wa Nigeria, licha ya kuondolewa, ilionesha soka la kuvutia na ushindani wa hali ya juu, lakini ikakosa umakini katika hatua ya mwisho ya penalti.
Morocco sasa inajiandaa kukutana na Senegal katika mchezo wa fainali utakaochezwa Januari 18, 2026, mechi inayotarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa kutokana na historia, ubora wa vikosi na uzoefu wa timu hizo katika mashindano ya kimataifa.
Mashabiki wa soka barani Afrika wanasubiri kwa hamu kuona ni nani atakayenyanyua taji la AFCON 2025, huku Morocco ikisaka kuongeza heshima yake barani Afrika na Senegal ikilenga kuendeleza ubabe wake katika soka la kisasa la Afrika.
