NA DIRAMAKINI
LIGI Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL) msimu wa 2025/2026 inaendelea kushika kasi huku ushindani mkali ukijitokeza katika nafasi za juu na chini ya msimamo wa ligi baada ya michezo ya raundi ya 10.
Simba Queens wanaendelea kuongoza ligi wakiwa kileleni mwa msimamo huo, baada ya kucheza michezo 10, kushinda mechi tisa na kutoka sare moja bila kupoteza mchezo wowote.
Aidha, mabingwa hao wa kihistoria wamekusanya pointi 28, wakifunga mabao 21 na kuruhusu mawili pekee, hali inayoonesha uimara mkubwa wa safu yao ya ulinzi na ushambuliaji.
Yanga Princess wanawafuatia kwa karibu Simba Queens wakiwa nafasi ya pili, wakikusanya pointi 27 baada ya kushinda michezo tisa kati ya 10 waliyocheza.
Pia, Yanga Princess wanaongoza kwa idadi ya mabao yaliyofungwa (31), ingawa wameruhusu mabao tisa na kupoteza mchezo mmoja.
Nafasi ya tatu inashikiliwa na JKT Queens wenye pointi 20, wakicheza michezo tisa, huku Alliance Girls wakikaa nafasi ya nne wakiwa na pointi 19.
Fountain Gate Princess wapo nafasi ya tano kwa pointi 16, wakionesha ushindani wa kati unaoendelea kuimarika kadri ligi inavyosonga mbele.
Katika nafasi za kati ya msimamo, Mashujaa Queens, Bunda Queens na Geita Queens wanaendelea kupambana kujinusuru na kushuka daraja, kila timu ikijitahidi kuboresha matokeo yao katika michezo ijayo.
Tausi FC na Ceasiaa Queens wapo katika hatari ya kushuka endapo hawatabadilisha mwenendo wa matokeo yao.
Kwa upande wa mkiani mwa msimamo, Bilo FC na Ruangwa Queens wanashika nafasi za mwisho (11 na 12) zenye hatari ya kushuka daraja.
Bilo FC ana pointi nne huku Ruangwa Queens akiwa na pointi tatu pekee, hali inayowalazimu kupambana kwa nguvu zote katika michezo iliyosalia ili kuepuka adhabu ya kushuka daraja.
Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania msimu wa 2025/2026 inaendelea kudhihirisha ukuaji wa soka la wanawake nchini, huku ubora wa ushindani, idadi ya mabao na mvuto wa ligi ukiendelea kuongezeka kadri raundi zinavyosonga mbele.
