KILIMANJARO-Afisa Uhamiaji Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro Mrakibu wa Uhamiaji, SI Sara Odunga, ametoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu na vigezo vinavyotakiwa ili kupata pasipoti ya kusafiria, akisisitiza umuhimu wa kufuata miongozo rasmi ya Idara ya Uhamiaji.
Akizungumza na wananchi mapema wiki hii Wilayani Mwanga kupitia kituo cha redio Kariongo Fm, SI Odunga amesema mwombaji wa pasipoti anatakiwa kuwa raia wa Tanzania na kuwa na nyaraka halali ikiwemo kitambulisho cha Taifa (NIDA) au namba ya NIDA, cheti cha kuzaliwa pamoja na barua ya utambulisho kutoka serikali ya mtaa au kijiji anachoishi.
Ameeleza kuwa, maombi ya pasipoti hufanyika kwa njia ya mtandao kupitia mfumo rasmi wa Idara ya Uhamiaji, na mwombaji anatakiwa kujaza taarifa sahihi pamoja na kulipia ada husika.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wenye uhitaji wa kusafiri nje ya nchi kuhakikisha wanaanza mchakato wa maombi ya pasipoti mapema iwezekanavyo kabla ya safari sanjari na kuhakikisha eanakuwa na nyaraka zote Muhimu zonazohitakika katika upatikanaji wa Pasipoti hizo.
Elimu hiyo imelenga pia kuongeza uelewa kwa wananchi wa Wilaya ya Mwanga kuhusu taratibu sahihi za kupata pasipoti ya kusafiria kwa mujibu wa sheria.
