ZANZIBAR-Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi inaendelea kushirikiana na wadau wa uvuvi kutoka nchi mbalimbali ili kutokomeza uvuvi haramu unaosababisha uharibifu wa mazingira ya baharini na kuathiri rasilimali za viumbe wa bahari.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mhe. Mboja Ramadhan Mshenga, wakati akifungua Mkutano wa Kikanda wa Sauti ya Buluu (Blue Voices) uliofanyika katika Hoteli ya Verde, Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema mkutano huo una lengo la kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na uvuvi haramu, sambamba na kukuza na kulinda Uchumi wa Buluu kwa maslahi ya nchi zinazozunguka Bahari ya Hindi.
Mhe. Mboja ameeleza kuwa ni muhimu kuboresha ushirikiano uliopo baina ya nchi zenye ukanda wa bahari ili kuhakikisha rasilimali za bahari zinalindwa, mazingira yanahifadhiwa na shughuli za baharini zinaendelea kuchangia maendeleo ya kiuchumi.
Amefafanua kuwa mkutano huo pia unajadili sera na sheria za baharini kwa lengo la kuzifanyia marekebisho na kuziimarisha ili kuwa nguzo madhubuti ya utekelezaji, huku akiwataka wavuvi kuitumia rasilimali ya bahari kwa uangalifu na kwa maslahi mapana ya Taifa.
Amesema uvuvi haramu unaathiri moja kwa moja uwepo wa viumbe wa baharini, hususan samaki wadogo wadogo, hali inayosababisha kupungua kwa rasilimali hizo na kuchangia mabadiliko ya tabianchi katika mazingira ya bahari.
Aidha, Naibu Waziri amesisitiza kuwa samaki ni rasilimali inayoweza kuisha endapo haitatunzwa, hivyo ni wajibu wa wote kulinda na kuhifadhi rasilimali za bahari kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Msemaji wa Mradi wa Jahazi, Bw. Michael Mallya, amesema lengo la mkutano huo ni kuzikutanisha Serikali za nchi zinazoshirikiana kutumia Bahari ya Hindi, hususan nchi za Afrika Mashariki na ukanda wa Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi, ili kujadili namna bora ya kukabiliana na uvuvi haramu na kuimarisha maendeleo ya baharini.
Ameeleza kuwa changamoto kubwa ni uvuvi unaofanywa na meli kubwa za uvuvi wa bahari kuu (deep sea fishing) kutoka nje ya nchi, ambazo husababisha kupungua kwa samaki na kuharibu miundombinu na ikolojia ya bahari.



