Mwezi Mtukufu wa Ramadhan si kisingizio cha kupanda bei za bidhaa-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa hakuna uhaba wa bidhaa za chakula nchini, hivyo wafanyabiashara hawana sababu ya kupandisha bei za bidhaa wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Rais Mwinyi ameyasema hayo Januari 30,2026 aliposhiriki Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyosaliwa katika Msikiti wa Fatma Bint Issa uliopo Kidongo Chekundu, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesisitiza kuwa, Mwezi wa Ramadhan haupaswi kuwa chanzo cha ongezeko la bei za bidhaa, bali ni mwezi wa rehema, huruma na kujikurubisha zaidi kwa Mwenyezi Mungu.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amewahimiza wananchi wenye uwezo kuwasaidia wanyonge na wasio na uwezo, hususan katika kipindi hiki cha ibada.

Alhaj Dkt. Mwinyi amesema,Serikali tayari imetoa maelekezo kwa Tume ya Ushindani Halali wa Biashara Zanzibar kuhakikisha kuwa bei za bidhaa muhimu za chakula ikiwemo mchele, unga wa ngano na sukari hazipandishwi wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, kwani bidhaa hizo zinapatikana kwa wingi nchini.

Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza Waumini wa Dini ya Kiislamu kusaidiana na kujiandaa vema kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, huku akiahidi kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha watu wenye uwezo kuwasaidia wasio na uwezo.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, amekemea tabia ya kuuhusisha Mwezi wa Ramadhan na michezo pamoja na matukio ya anasa, akisisitiza umuhimu wa kuuheshimu mwezi huo kwa kuzingatia ibada na maadili ya Kiislamu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here