Naibu Waziri wa Fedha atembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana (DIB)

TANGA-Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula, ametembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana (DIB) tarehe 21 Januari 2026 katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Usagara jijini Tanga na kupokelewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Bw. Lwaga Mwambande na Mwanasheria wa DIB, Esther Mpendaamani.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (katikati) akifuatana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bw. Dadi Kolimba na kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi Dionisia Mjema, wakati walipowasili katika banda la Bodi ya Bima ya Amana inayoshiriki Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa tarehe 21 Januari 2026 na kupokewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Bw. Lwaga Mwambande na Mwanasheria wa DIB, Bi. Esther Mpendaamani.

Katika banda hilo, Mheshimiwa Naibu Waziri amepewa maelezo kuhusu majukumu ya DIB yakiwemo wajibu wa kukinga amana za wateja wa benki na taasisi za fedha zenye leseni ya Benki Kuu, kutathmini na kukusanya malipo ya bima/michango kutoka katika benki na taasisi za fedha; kusimamia Mfuko wa Bima ya Amana; na kulipa fidia kwa wenye amana pale ambapo benki au taasisi ya fedha inapofilisika.

Katika uwasilishwaji Mheshimiwa Naibu Waziri alifahamishwa zaidi juu ya majukumu mengine ya Bodi ya Bima ya Amana ambayo ni kusimamia ufilisi wa benki na taasisi ya fedha kama Bodi ya Bima ya Amana itateuliwa na Benki Kuu ya Tanzania kufanya kazi hiyo; na kupunguza hasara inayoweza kupatikana kwa benki au taasisi ya fedha kufungwa kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania, jukumu ambalo lipo kwenye utekelezaji.

Aidha, Bw. Mwambande, alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa waliokuwa na amana katika iliyokuwa benki ya FBME ambayo iko katika ufilisi, kuchangamkia fursa ya kupata fidia yao ya awamu ya tatu ya asilimi 30 ya fedha zao.

Fidia hii ambayo ilitangazwa mwezi Novemba 2025, inafanya hadi sasa wenye amana hao waliopo hapa nchini kuwa wamelipwa fidia ya asilimia 85 ya amana zao. Awali, walilipwa asilimia 55 katika awamu mbili za kwanza.
Katika ziara yake DIB, Naibu Waziri, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maadhimisho haya kwa niaba ya Waziri wa Fedha, alifuatana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba.

Bodi ya Bima ya Amana iko katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yenye kauli mbiu ya ‘’Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi,” ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yao, na kuwahakikishia kwamba wanapofungua akaunti benki au taasisi ya Fedha iliyosajiliwa na yenye leseni ya Benki Kuu, watambue kwamba tayari amana zao zina kinga kupitia DIB.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here