NHC 2026:Enzi ya mipango yafungwa,ni mwendo wa matokeo tu

DAR-Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linaingia mwaka 2026 likiwa kwenye awamu mpya ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya makazi na biashara, likilenga kuboresha maisha ya Watanzania na kuchochea maendeleo ya miji kwa vitendo vinavyoonekana.
Akitoa Salamu za Mwaka Mpya kwa wafanyakazi na wadau wa Shirika, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah Hamad, amesema, mwaka 2026 ni mwaka wa kasi, utekelezaji na matokeo, ambapo msisitizo utawekwa katika kukamilisha miradi inayoendelea na kuanzisha miradi mipya ya makazi bora na ya gharama nafuu.

“Mwaka 2026, NHC haiongei tena mipango; inaongea matokeo,” amesema Bw. Hamad.

Kwa mujibu wake, NHC imeendelea kuimarika kifedha, ambapo thamani ya mali za Shirika imeongezeka kutoka shilingi trilioni 5.4 mwaka 2024 hadi zaidi ya shilingi trilioni 6 mwaka 2025. Ukuaji huu umeiwezesha NHC kuongeza kasi ya ujenzi, kuwekeza zaidi kwenye miradi ya kimkakati, kulipa kodi kwa Serikali na kuongeza gawio kwa Taifa.

Katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora na yenye staha, NHC inaendelea na utekelezaji wa miradi ya nyumba za makazi ikiwemo Samia Housing Scheme, unaolenga kujenga nyumba 5,000 za gharama ya kati katika maeneo mbalimbali nchini. Tayari nyumba 560 zimekamilika Kawe, Dar es Salaam, na wanunuzi wameanza kukabidhiwa na kuhamia katika makazi yao mapya.

Ujenzi wa Samia Housing Scheme unaendelea pia katika maeneo ya Kijichi, Medeli, Iyumbu na maeneo mengine, sambamba na maandalizi ya kuanzisha miradi mipya ya makazi katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Ruvuma na Kagera.

Mbali na makazi, NHC inaendelea kutekeleza miradi ya majengo ya biashara na miradi ya makazi na biashara mchanganyiko (mixed-use developments) katika miji mbalimbali ikiwemo Morogoro, Tanga, Iringa, Tabora, Singida, Bukoba, Masasi, Lindi na Mtwara, kwa lengo la kuongeza mapato, kufungua ajira na kuimarisha uchumi wa maeneo husika.

Bw. Hamad ameongeza kuwa NHC imechukua hatua za kimkakati kuboresha huduma kwa wateja kwa kuanzisha NHC Mobile App, itakayowezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi na uwazi. Aidha, maandalizi ya Nyumbani Bond yanaendelea, mpango utakaowawezesha wananchi na taasisi kuwekeza moja kwa moja katika ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.

“Tunajenga nyumba zenye viwango, katika maeneo yaliyopangiliwa, zenye thamani inayoongezeka kwa muda. Ndiyo maana wateja wanaendelea kuiamini NHC,” amesisitiza.

Kwa mwaka 2026, kipaumbele cha NHC ni kukamilisha miradi mikubwa iliyokuwa imesimama, kuimarisha sera ya ubia, kuendelea na matengenezo ya nyumba zilizopo na kuhakikisha huduma kwa wateja zinatolewa kwa uwazi, uadilifu na ufanisi.

Kwa ujumla, NHC inaendelea kujijenga kama taasisi ya kisasa, ya kibiashara na yenye mwelekeo wa wazi wa kujenga makazi bora, kukuza biashara na kuunga mkono maendeleo ya Taifa.

“NHC haijengi majengo pekee; inajenga maisha, inawezesha biashara na inaweka msingi wa maendeleo ya miji ya kesho,” amehitimisha Bw. Hamad.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here